MLINDA mlango wa JKT Tanzania, Aboubakar Barwany amesema kipa yeyote duniani asingeweza kuokoa mpira wa ‘frii-kiki’ uliopigwa Bernard Morrison ‘BM33’ katika pambano la Yanga na Simba lililopigwa Jumapili iliyopita.
Morrison alipiga mpira huo uliopita juu ya ukuta wa Simba na kwenda kuingia wavuni kupitia ‘anapotagia ndege’na kuipa Yanga uahindi wa kwanza wa ‘Dabi ya Kariakoo’ tangu 2016.
Alisema hata kama kipa Aishi Manula angeweza kuucheza mpira huo basi sasa hivi angekuwa anauguza majeraha kwani Morrison aliupigwa sehemu mbaya sana.
Barwany alisema kipa yeyote kamwe asingeweza kucheza faulo ile kwani Morrison alitumia akili nyingi kupiga ‘frii-kiki’ ile kwani aliwadanganya mabeki hadi Manula wasijue atapigia upande upi.
“Unawezaje kucheza ule mpira na kama Manula angeufuata na kupangua basi asingeweza
kuendelea na mechi kwani angeumia kwa sababu Morrison aliupigia sehemu mbaya sana na angeweza kujigonga kwenye mlingoti na kuumia,” alisema Barwany.
Alisema hata hivyo Manula anahitaji pongezi kwani aliweza kuufata mpira huo na kwamba kwa jinsi ulivyopigwa, makipa wengi huishia kuutazama tu na kuganda sakafuni kama vile wamepigiliwa misumari.
“Kwangu nampongeza kipa kwani alijaribu kwa uwezo wake wote kuufuata ule mpira lakini haikuwezekana. Kikubwa mashabiki wa soka wajue lile bao anafungwa kipa yeyote duniani na wasije kumlaumu kabisa Manula,” alisema kipa huyo.
No comments:
Post a Comment