
Dar es Salaam. Kila mchezaji wa Yanga atavuna zaidi ya Sh6 milioni endapo timu hiyo itaifunga Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Jumapili wiki hii.
Yanga na Simba zitavaana katika mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi hiyo baada ya awali kutoka sare ya mabao 2-2. Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Iko hivi. Yanga kupitia wadhamini wake Kampuni ya GSM imeahidi kutoa Sh200 milioni kwa wachezaji endapo watashinda.
Timu hiyo imesajili wachezaji 30, hivyo zikigawanywa kila mchezaji atapata Sh6.6 milioni ikiwa ni ahadi ambayo haikuwahi kutolewa na kiongozi au mfadhili yeyote wa klabu hiyo.
Yanga imetoa taarifa hiyo ikiwa ni muda mfupi baada ya watani wao wa jadi Simba kuahidi kumpa kila mchezaji atakayecheza bila kujali dakika ngapi atapata Sh4 milioni endapo watashinda mchezo huo.
Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz alisema GSM imetoa ahadi hiyo ili kuongeza morali kwa wachezaji.
“Hata Simba wakichukua ubingwa si tatizo, tunachohitaji ni kuwafunga nadhani raha ya ubingwa itakuwa imeisha.
“Tulikuwa na utaratibu wa kutoa motisha kila wanaposhinda mechi ya Ligi Kuu hupewa milioni 10 lakini kutokana na umuhimu wa mchezo wa Jumapili tumeamua kufanya kitu kwa wachezaji,”alisema Nugaz.
Alisema kocha Luc Eymael ameisoma Simba na amebaini kasoro zao ambazo atatumia kupata ushindi katika mchezo huo.
“Luc atashambulia mwanzo mwisho na Charles Mkwasa ( kocha msaidizi wa Yanga) amemueleza vitu vingi kuhusu mchezo huo,”aliongeza.
Mara ya mwisho Yanga kuifunga Simba ilikuwa Februari 20, 2016 iliposhinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Donald Ngoma na Amissi Tambwe.
Baada ya mechi hiyo timu hizo zimekutana mara tano na katika michezo hiyo Simba imeshinda miwili mabao 2-1 Februari 26, 2017 yaliyofungwa na Laudit Mavugo 66 na Shiza Kichuya. Simon Msuva alifunga kwa Yanga.
Februari 16, mwaka jana Simba ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Meddie Kagere.
No comments:
Post a Comment