
LONDON,ENGLAND .SIKU kadhaa zimepita huku kukiwa hakuna taarifa yeyote juu ya lini Ligi Kuu England itakuwa inaanza, hii imesababisha baadhi ya wachezaji kukaa majumbani kwao na kujifanyia mazoezi ya kujiweka tayari iwapo ligi hiyo itakuwa imeanza tena kutimua vumbi.
Hawa ni baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa wakijifua vilivyo ili kujiweka tayari na mashindano hayo yatakapo rudishwa tena.
1. David Luiz
Beki huyu kitasa wa Arsenal ameonekana kujifua vilivyo akiwa nyumbani kwake. Ikiwa ni mojawapo ya njia ya kujiweka tayari iwapo ligi hiyo itaanza tena. Kwa sasa timu yake ya Arsenal imesimamisha mazoezi na shughuli zote kutokana na hatari ya virusi vya corona vilivyo ripotiwa kumkumba kocha wa klabu hiyo, Mikel Arteta wiki iliyopita.
2. Theo Walcott
Straika huyu wa zamani wa Arsenal ambaye kwa sasa anaitumikia Everton ameonekana kwenye picha tofauti tofauti kwenye mitandao ya kijamii, akiwa anapiga tizi la haja.
Picha hizo zilikuwa zilimuonesha akiwa gym ambako alikuwa anafanyia mazoezi ya aina mbalimbali. Hii ilikuwa ni siku ya Jumatano asubuhi alikuwa ananyanyua vyuma vizito baada ya kufanya mazoezi mengine magumu ili kujiweka fiti.
3. Nicolas Otamendi
Kitasa huyu wa Manchester City, alionekana akiwa kwenye sehemu ya mazoezi iliyopo nyumbani kwake, picha zilimuonesha akiwa anafanya mazoezi ya kunyanyua vyuma vizito kupitia mashine iliyokuwepo kwenye chumba hicho.
4. Sadio Mane na Segbe Akanpo
Mastraika hawa waawili wote kwa pamoja walionekana wakiwa kwenye tizi zito la kujiweka sawa na Ligi Kuu iwapo itarudishwa tena.
Mane alionekana akiwa na anafanya mazoezi ya kukimbia kwenye mashine maalumu ya akiwa na mchezaji wa Oldham Athletic, Segbe Akanpo, ambaye ndiye aliyeweka picha kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram iliyowaonesha wawili hao wakiwa mazoezini.
5. Christian Pulisic
Kiungo huyu mshambuliaji wa Chelsea ameonekana kujiweka fiti baada ya kutoka kwenye majeraha ya misuli aliyoyapata Januari mwaka huu. Anafanya mazoezi nyumbani kwake katika kipindi hiki ambacho klabu yake haifanyi mazoezi. Hii imetokea baada ya kikosi kizima cha Chelsea kuzuiwa kuendelea na shughuli za kawaida za kitimu kufuatia straika wa timu hiyo Callum Hudson-Odoi, kukutwa na mambukizi ya virusi hivyo.
6. Florian Lejeune
Beki huyu anachezea Newcastle United naye pia alionekana kufidia muda ambao anaukosa kufanya mazoezi na timu, kwa kuamua kufanya kukimbia akiwa nyumbani kwake. Ikiwa ni moja ya njia ya kujiweka sawa iwapo Ligi Kuu England itakuwa imeruhusiwa kuendelea tena.
Wakati wachezaji hawa wanajifua vikali na kujiweka fiti kuna baadhi ya wachezaji wao wametulia zao majumbani mwao wakiendelea kula bata tu.
Mmoja kati ya wachezaji wa klabu ya Buyern Munich, Jerome Boateng ameonekana kutojali na kuendela kula maisha baada ya kuonekana akiwa anapiga danadana kwa kutumia karatasi za choon.
Hii ni mojawapo ya michezo iliyoanzishwa kwenye mitandao ya kijamii na kupewa jina la #Stayathomechallenge.
Mchezaji mwengine anayecheza Ujerumani aliyeonekana kufanya mchezo huo ni Leon Biley. Mchezo huu umekuwa ukifanywa na wachezaji wengi barani Ulaya.
No comments:
Post a Comment