
Dar es Salaam. Wakati KMC ikiendeleza wimbi la ushindi katika mechi yake ya tatu mfululizo, kocha wa Yanga, Luc Eymael amesema furaha ya Simba imewagharimu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, kocha huyo alisema kipigo cha bao 1-0 ilichopata dhidi ya KMC, kilichangiwa na uchovu wa furaha.
Eymael alisema ingawa KMC ni timu nzuri, lakini wachezaji wake hawakuwa makini katika maandalizi ya mchezo huo.
“Tumepata matokeo mabaya ambayo hatukutegemea, hii imechangiwa na furaha ambayo walikuwa nayo wachezaji baada ya kuifunga Simba
“Hata hivyo tumecheza na timu bora ambayo licha ya kuwa katika nafasi ya chini ina wachezaji hodari wanaojituma,”alisema kocha huyo raia wa Ubelgiji.
KMC imeongeza kasi ya kukwepa panga la kuteremka daraja baada ya kuichapa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa matokeo hayo, KMC imechupa hadi nafasi ya 16 katika msimamo wa ligi baada ya kufikisha pointi 30.
Pia ushindi huo ni wa tatu mfululizo ambapo awali iliichaoa Mbao ya Mwanza mabao 2-0 kabla ya kuilaza JKT Tanzania bao 1-0.
Bao pekee la mshambuliaji Salim Aiyee aliyefunga kwa kiki ya mguu wa kushoto baada ya kuitoka ngome ya Yanga, limefufua matumaini ya KMC kupigania nafasi ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao.
Mchezaji huyo aliyekuwa nje ya uwanja muda mrefu kutokana na majeraha, alifunga bao hilo dakika ya 62.
Mechi hiyo ilichezwa kwa mbinu nyingi na makocha wote wawili waliingia kwa kuwapa maelekezo wachezaji wao kucheza kwa nidhamu.
KMC ilianza na mfumo wa 4-1-3-2 wakitumia mabeki wanne, kiungo mkabaji mmoja, viungo washambuliaji watatu na washambuliaji wawili.
Mfumo huo uliisaidia KMC kucheza kwa nidhamu katika kuzuia kwani licha ya kwamba kipindi cha kwanza Yanga ilipata nafasi za kufunga lakini ilishindwa.
Licha ya kuzuia mashambulizi ya Yanga yaliyopitia kwa Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima na Mapinduzi Balama ilishindwa kufunga.
Yanga ilianza kwa mfumo wa 4-4-2 unaotumia mabeki wanne, viungo wanne na washambuliaji wawili ambao walicheza Nchimbi na Niyonzima.
Timu hiyo ilitengeneza mashambulizi mengi eneo la katikati akicheza Papy Tshishimbi, Feisal Salumu na pembeni Patrick Sibomana.
Kipa wa KMC Jonathan Nahimana alikuwa kikwazo kwa Yanga baada ya kuokoa kiki kadhaa za washambuliaji wa Yanga waliokuwa wakisaka mabao.
No comments:
Post a Comment