
Nyon, Uswis .MASTAA wa zamani wa Arsenal, Johan Djourou na Alex Song ni miongoni mwa wachezaji tisa wa klabu ya Sion ya Ligi Kuu Uswis waliovunjiwa mikataba.
Mbali na Song na Djourou, wengine walivunjiwa mikataba ni nahodha wa klabu hiyo Xavier Kouassi, Pajtim Kasami, Ermir Lenjani, Seydou Doumbia, Mickael Facchinetti, Christian Zock na Birama Ndoye.
Uamuzi wa kuvunjiwa mikataba kwa wachezaji hao imetokana na kugoma kukatwa sehemu ya mishahara wakati huu ambao, ligi karibu zote barani Ulaya, Afrika na Amerika zimesimama kutokana na tishio la kusambaa kwa virusi vya corona.
Kwa sasa klabu nyingi zimekuwa zikipata hasara kutokana na kukosa mapato yanayotokana na haki za televisheni, mauzo ya vifaa vya michezo na mapato ya milangoni kutokana na ligi kusimama kwa muda hadi hapo mambo yatakapokaa sawa.
Rais wa Sion, Christian Constantin anatajwa kuwa ameajiri zaidi ya makocha 40 tangu alipochukua uongozi klabuni hapo mwaka 2003, akiwemo kocha wa sasa wa Napoli, Gennaro Gattuso.
Mwaka 2011, Sion iliondolewa kwenye michuano ya Europa League na kusababisha majanga huku miaka miwili baadaye wakafungiwa kushiriki michuano ya Ulaya.
Song na Djourou wamepata kuwa wachezaji muhimu kweye kikosi cha Arsenal wakati huo ikiwa chini ya Arsene Wenger, ambaye kwa sasa ni mshauri wa Shirikisho la Soka Duniani, Fifa.
No comments:
Post a Comment