
LONDON, ENGLAND . MANCHESTER United wameambiwa wachague moja kupigwa mkwanja mrefu kwa kumsajili Jadon Sancho au wabane matumizi kwa kwenda kunasa tu huduma ya staa wa Aston Villa, Jack Grealish.
Mtaalamu mmoja wa masuala ya kipesa alisema Sancho anakuzwa sana sokoni, akiuzwa bei mbaya baada ya klabu yake ya Borussia Dortmund kuhitaji Pauni 120 milioni, wakati Grealish anaweza kupatikana kwa Pauni 60 milioni tu, ambapo kuna chenji nyingine nyingi inabaki ya kufaa kusajili mchezaji mwingine wa nguvu kama vile James Maddison wa Leicester City au Moussa Dembele wa Lyon.
Man United wenyewe wanamtaka Sancho, lakini wameambiwa kwamba kunasa saini yake itabidi kwanza wahakikisha wanafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, la sivyo watamsikia tu redioni akienda kwa mahasimu wao Liverpool.
Kinda huyo wa miaka 19, Sancho anafukuziwa pia na Chelsea wakihitaji saini yake akafanye mambo huko Stamford Bridge.
Kwa mujibu wa Sky Sports, Sancho yupo kwenye rada pia za Liverpool akitakiwa na kocha Jurgen Klopp, ambaye aliwahi kuinoa Dortmund. Lakini, Man United wao wana uhakika mkubwa kwamba watanasa saini yake na atatua Old Trafford.
Hata hivyo, jeuri yote ya Man United itatimia kama tu watafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, jambo ambalo ndilo lililowakamisha kwenye mpango wa kumsajili straika mtambo wa mabao Erling Haaland, aliyetimkia zake Dortmund.
Kukosekana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu ndicho kitu kilichowafanya Man United wakose huduma ya Haaland licha ya maelezo ya kocha Ole Gunnar Solskjaer kwamba straika huyo wa Norway alihitaji kwenda zake Old Trafford kabla ya kubadili mawazo.
Man United kwa sasa inashika nafasi ya saba kwenye msimamo, pointi tatu nyuma ya Chelsea waliopo kwenye nafasi ya nne.
Solskjaer alisema: “Ligi ya Mabingwa inaipa klabu machaguo mengi zaidi, pesa zaidi. Ni michuano yenye hadhi kujihusisha nayo. Kama tutacheza vizuri hadi mwisho wa msimu, itakuwa jambo rahisi. Ila siamini pia kama msimu ujao tuwepo au tusiwepo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya basi itakuwa mwisho wa wachezaji kuja kujiunga na sisi.”
No comments:
Post a Comment