Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi aliyesimama akizindua Jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Singida. Kushoto ni Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP) Nchini, Biswalo Mganga na kulia in Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angerina Lutambi
Picha ya pamoja baina ya Mkrugenzi wa Mashitaka,(DPP) Biswalo Mganga mwenye suti , Mkuu wa Mkoa wa Singida (mwwnye kilemba) anayefuata Dkt.Angelina Lutambi Katibu Tawala Mkoa wa Singida na wajumbe wa Jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Singida Mara baada ya kuzinduliwa kwa Jukwaa hilo la Mkoa
Baadhi ya watumishi wa Umma Singida walioshiriki kwenye uzinduzi wa Jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Singida( Picha Zote na John Mapepele,Singida
Na John Mapepele, Singida
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amezindua Jukwaa la Mkoa la Haki Jinai leo huku Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Nchini, Biswalo Mganga akisema kuwa uzinduzi huu unafanywa kitaifa mkoani Singida na kuelekeza mikoa yote nchini kuzindua ili kusaidia kupambana na uhalifu wa kijina katika mikoa husika hivyo kupunguza mrundikano wa mahabusu.
Dkt. Nchimbi amesema kuzinduliwa kwa Jukwaa hili kutakuwa nguzo kuu ya kuzima uhalifu katika Mkoa wa Singida, huku akiwataka wajumbe kutumia jukwaa hili kufanya utatifi na kutafakari kwa kina ni namna gani bora ya kudhibiti uhalifu badala ya kusubili utokee na kupeleka kesi mahakamani, jambo ambalo amesema madhara yake yamekuwa makubwa.
“Namshukuru Mungu. Leo, kwangu ni siku ya kihistoria na ya kipekee ambayo nilitamani kuona inatimia tangu siku nyingi. Kila wakati nimekuwa nikiwasisitiza kuwa ni muhimu na ni lazima vyombo vyote vya Serikali katika mkoa wetu kufanya kazi ya kupambana na uhalifu kwa pamoja badala ya kila mmoja kujiona ni bora zaidi katika nafasi yake jambo halina tija na halitusaidii kama taifa, lakini hatimaye leo hili linatimia” alisisitiza
Aidha amewataka Wajumbe kufanya kazi kwa umoja na uzalendo ili jukwaa hilo liwe mfano bora na mikoa mingine waje kujifunza.
“Kama kwenye mambo mengine tumeweza kushika nafasi za kwanza kitaifa kwa nini tusiwe wa kwanza katika kufanya kazi nzuri kwenye kutekeleza majukumu ya jukwaa la Haki Jinai kwenye Mkoa wetu na wengine waje kujifunza kwetu, inawezekana endapo kila mtu atatekeleza wajibu wake” alisisitiza Dkt. Nchimbi
Dkt. Nchimbi amesema hata vitabu vitakatifu vimeandika mwisho ya uhalifu ni mbaya na kwamba msharaha wa dhambi ni mauti na kuelekeza kuwa kila Ofisi na Idara ya Serikali katika Mkoa wa Singida kuwa na mfumo wa Jukwaa la Haki Jinai ambao utasaidia kujenga mfumo wa kutafakari na kudhibiti uhalifu badala ya kusubiri utokee.
Amesema ili kuwa na ufanisi na tija wa kutokomeza uhalifu kwenye Mkoa wake ameyataka majukwaa ya Haki Jinai ya kila Wilaya kuanza mara moja kufanya kazi na kupeleka mapendezo yake katika Jukwaa la Mkoa kwa kuwa Jukwaa la Mkoa linategemea utendaji wa majukwaa ya Wilaya.
Akizungumza katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kabla ya uzinduzi huo , Mganga amesema kwa mujibu wa Sheria ya Mashitaka na 27 ya mwaka 2008 ibara ya 59(B) (II) na kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Mkurugenzi wa Mashitaka ndiye mwenye jukumu la kuratibu upepelezi wa kesi zote za jinai nchini japokuwa anaweza kukasimu madaraka hayo kwa vyombo vingine vya Serikali.
Amesema Ofisi yake imedhamilia kutokomeza uhalifu wa kijinai kwa kutekeleza mkakati wa kuunda kwa majukwaa ya Haki Jinai kila Mkoa hapa nchini ambalo ni takwa la kisheria ili kuwa muarobani wa kuthibiti matukio na kesi za kijinai badala ya kusubiri makosa yafanyike na kutoa hukumu jambo ambalo amesema halina tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Mganga amesema kwa kuzingatia ukubwa wa tatizo na ongezeko wa uhalifu wa kijinai Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais, John Pombe Joseph Magufuli iliamua kufanya marekebisho makubwa ya kupambana na tatizo hili ambapo iliunda Ofisi ya Taifa ya Mashitaka kwa kutangaza kwenye gazeti la Serikali namba 49, tarehe 13/2/2018 tofauti na awali ambapo Kurugenzi ya Mashitaka (DPP) ilikuwa chini ya Ofisi ya Mwanasherioa Mkuu wa Serikali.
Amewataka wajumbe wote wanaounda jukwaa hilo kufanya kazi kwa weredi na kushirikiana ili kuhakikisha mazingira ya shughuli za kijinai yanakwenda vizuri ambapo amesema majukwaa ya Mkoa yanatakiwa kutoa mapendekezo ya nini kifanyike kwenye Jukwaa la Haki Jinai la Taifa kwa ajili ya utekelezaji na ufuatiliaji.
Amesema kuliungana na Sheria ya Mashitaka, Jukwaa la Haki Jinai la Mkoa linatakiwa kukaa vikao visivyopungua viwili kwa mwaka ambapo amesisitiza wajumbe kuhudhuria wao wenyewe badala ya kuja wawakilishi kwa kuwa sheria inawataka wajumbe halisi na sio wawakilishi na kuongeza kuwa kama kunakuwa na ulazima au umuhimu, vikao hivyo ninaweza kuketi zaidi ya mara mbili kwa mwaka kadri ya mahitaji.
Mkurugenzi, Mganga ameelekeza Jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Singida kuanza kazi mara mmoja ili kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili uhalifu katika mkoa ambapo amelitaka kuketi mara mbili kabla ya Oktoba mwaka
Mwenyekiti wa Jukwaa la Mkoa wa Singida, Rose Chilongozi ambaye ni Mwendesha Mashitaka Mkoa wa Singida alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa kuzindua Jukwaa hilo na kumhakikishia kuwa yeye na wajumbe wake watafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kudhibiti uhalifu katika mkoa huo.
Katibu wa Jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Singida ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Mkoa huo, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Stela Mutabihirwa amewataja wajumbe wa Jukwaa hilo kuwa ni pamoja na Mwendesha Mashitaka wa Mkoa ambaye ni Mwenyekiti, Mkuu wa upelelezi wa Mkoa ambaye ni Katibu, Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Mkoa,
Wengine ni Afisa Ustawi wa Mkoa, Mwenyekiti wa Bodi ya Parole wa Mkoa, Afisa Mkemia Mkuu wa Mkoa, Afisa-Bwana Huruma wa Mkoa, Mwanasheria kutoka Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa na Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa na mdau mwingine yoyote ambaye wataona anafaa kumwalika kushughulikia jambo husika.
Kamishina Msaidizi wa Polisi Mutabihirwa ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Singida amesema kwa upande wa Polisi anaishukuru Serikali kwa kuharakisha kuzindua jukwaa hilo kwenye Mkoa wa Singida kwa kuwa litasaidia kutatua changamoto mbalimbali za uhalifu.
“Napenda kumshukuru Mheshimiwa, Rais Magufuli kwa kuunda chombo hiki kupitia Ofisi ya Mashitaka kwani kwa sisi Jeshi la Polisi tutashikisha dawati letu la Polisi Jamii ambapo sasa naamini tutatoa elimu mashuleni na kupunguza mimba za utotoni pia uhalifu wa mauaji, ukatili wa kijinsia na migogoro ya ardhi na mashamba ya wananchi katika Mkoa wetu itapata ufumbuzi wa kudumu” ameongeza Afande Mutabihirwa
Akifungua rasmi kikao cha uzinduzi wa Jukwaa hilo Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi amesema kila mwananchi anawajibu wa uzuia uhalifu ili Mkoa wa Singida uwe sehemu salama.
Aidha aliwaasa wajumbe kufanya kazi kwa kuzingatia sheria ili kuwa ukuta imara wakuzuia aina yoyote ya uhalifu ambao unaweza kupenya na kuingia makao makuu ya nchi.



No comments:
Post a Comment