Search This Blog

Friday, February 7, 2020

Kumbe tatizo la waamuzi zito

By Mwandishi wetu

INAWEZEKANA makosa ya waamuzi wa soka nchini yakawa ni matukio yanayotokea kwa bahati mbaya, lakini muendelezo wake unazidi kuleta mshangao na kufanya watu wawe na fikra hasi dhidi yao.

Huu unaweza kuwa miongoni mwa misimu ya Ligi Kuu Bara ambayo imekuwa na idadi kubwa ya makosa ya waamuzi kwa kutoa maamuzi ambayo katika hali ya kushangaza ni yale yanayohusu matukio ambayo kwa macho ya kawaida hayaonekani kama yanaweza kumuweka refa katika wakati mgumu kuyaamua.

Iko mifano mingi ya waamuzi kuchemsha msimu huu katika kutafsiri baadhi ya sheria kati ya zile 17 zinazousimamia mchezo wa soka ambayo unaweza kutumia ukurasa mzima kuiorodhesha.

Ilianzia katika mechi za mwanzoni tu za ligi ambapo timu ya Ruvu Shooting ilinyimwa bao halali katika mchezo wake dhidi ya Yanga, lakini kwa mshangao wa wengi, mwamuzi msaidizi alinyoosha kibendera kuashiria mfungaji alikuwa ameotea wakati kwa hali halisi hilo halikuwepo.

Lakini, hayo yaliendelea katika michezo iliyofuata ya Ligi Kuu Bara ukiwemo ule wa Yanga dhidi ya Mbeya City wa Desemba 24, 2019 ambao mwamuzi Florentina Zabron aliwanyima Yanga nafasi mbili za kupata mikwaju ya penati baada ya Mbeya City kufanya faulo mbili za wazi katika nyakati mbili tofauti. Hata hivyo, katika hali ya kushangaza mwamuzi huyo hakutoa uamuzi uliotegemewa na wengi ama uliostahili.

Januari 4, mwaka huu, waamuzi wa mchezo wa Watani wa Jadi, Jonesia Rukyaa, Soud Lila na Hamis Chang’walu waliingia lawamani kwa kufanya makosa kadhaa ambayo yaliwafanya wazue mjadala mkali kuhusu uwezo wao.

Advertisement

Kitendo cha kuizawadia Simba mkwaju wa penati mara baada ya Kelvin Yondani kumchezea rafu Meddie Kagere nje ya eneo la hatari, lakini pia kutoona tukio la beki Pascal Wawa kumkanyaga kwa makusudi mshambuliaji Ditram Nchimbi, kilichochea utambi katika mjadala unaohusu waamuzi nchini.

Katika mchezo wa Kombe la Azam Sports Federation uliochezwa Uwanja wa Taifa mnamo Januari 25, Mwadui FC iliyokuwa ugenini kukabiliana na Simba ilinyimwa fursa muhimu ya kufunga bao, baada ya mwamuzi msaidizi kuonyesha kibendera cha kuashiria mchezaji Venance Ludovick aliotea ingawa kiuhalisia haikuwa hivyo.

Matukio hayo ni baadhi tu ya namna changamoto ya waamuzi ilivyo msimu huu na kwa bahati mbaya zaidi imekuwa ikiendelea kujirudia huku tatizo likiwa linazidi kuota mizizi.

Swali kubwa ambalo wengi wamekuwa wakijiuliza ni je makosa hayo yanafanyika kwa makusudi au bahati mbaya?

Kwa nia ya kusaidia kutafuta utatuzi wa tatizo hilo sugu la mfululizo wa waamuzi wa mpira wa miguu kufanya makosa ambayo yamekuwa na muendelezo, Mwanaspoti limefanya uchunguzi na kubaini mambo manne.

Mambo haya ndio yanawafanya ama kuwakwamisha waamuzi wa soka nchini kushindwa kutimiza majukumu yao na labda yanaweza kuwa chanzo cha kuyumba katika kuzitafsiri sheria za mchezo huo.

malipo kuchelewa

Waamuzi wa soka nchini wamekuwa wakipita katika kipindi kigumu msimu huu kutokana na kucheleweshewa posho zao za idadi kubwa ya mechi walizochezesha sambamba na fedha za gharama za nauli kutoka kituo kimoja hadi kingine.

Katika mazingira ambayo mwamuzi anatoka mkoa mmoja kwenda mwingine kuchezesha mechi huku akiwa hajalipwa chochote na kulazimika kujitegemea, inaweza isiwe jambo gumu kwake kurubunika na kuingia katika mtego wa rushwa na timu mojawapo kati ya anazozichezesha ili ainufaishe.

Inadaiwa kuwa baadhi ya waamuzi hasa wale wenye shughuli ambazo haziwaingizii kipato kikubwa wamekuwa wakisafirishwa, kulipiwa gharama za malazi na chakula sambamba na posho na klabu jambo ambalo huleta mgongano wa kimaslahi. Pengine hili limekuwa likitumika kuwalazimisha kuzibeba ili kulipa fadhila kwa msaada ambao wamepata.

Hata hivyo, taarifa ambazo gazeti hili linazo kutoka kwa waamuzi zinadai kuwa kwa sasa wamelipwa madai yao ya posho kwa mechi walizochezesha katika mashindano ya Kombe la Azam Sports Federation na zile za Ligi Kuu hadi raundi ya 12.

Waamuzi hao wamefichua kuwa fedha hizo wameingiziwa mara baada ya taarifa zao za kutolipwa kwa muda mrefu kusambaa ingawa mwanzoni zilifanywa kuwa siri kubwa.

“Tumelipwa lakini malipo hayo yameishia katika mechi za raundi ya 12 na zile za Kombe la FA, lakini hizo raundi zilizobakia hatujalipwa hadi sasa na hatujui lini tutalipwa. Kwa sasa mechi za Ligi Kuu Bara ziko mzunguko wa 19.

“Hili jambo limekuwa likituweka katika wakati mgumu kwa sababu unakuta refa unapangiwa mechi katika mkoa uliopo mbali, lakini hata nauli hupewi unaambiwa ujilipie kisha utarudishiwa.

“Mazingira kama hayo kama mwamuzi hajajipanga, inakuwa ni rahisi kurubunika kwa sababu hawezi kukacha kuchezesha na mabosi huwezi kuwaeleza lolote wakakuelewa ikiwa haujafika kituoni,” alisema mwamuzi mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina kwa kuhofia kuchukuliwa hatua na mamlaka.

Mwamuzi mwingine mzoefu wa ligi hiyo alifichua kuwa kucheleweshewa malipo yao kumesababisha hata baadhi yao kuondolewa katika orodha na wengine kushushwa madaraja pale ambapo wamekuwa wakiwasilisha madai yao.

“Kuna marefa wanadai hadi Sh7 milioni kutokana na malimbikizo ya michezo waliyochezesha, lakini hawana uhakika wa kulipwa fedha hizo zote na ukionekana uko mstari wa mbele kupigania haki yako, unajikuta umeshushwa daraja ama kuondolewa katika orodha ya waamuzi.

“Wenye mamlaka wametufunga midomo na ukitaka kuingia matatizoni basi uwe unazungumza au uonekane unaulizia kuhusu malipo hayo. Wengi wanalazimika kukaa kimya, lakini wanaumia na hasa wale marefa ambao hawana majina makubwa,” alisema mwamuzi huyo.

Uchanga wa waamuzi

Hii nayo imekuwa ikitajwa kuwa sababu nyingine ambayo imekuwa ikipelekea makosa ya mara kwa mara ya waamuzi msimu huu, kutokuwa na uzoefu wa kutosha. Utaratibu uliotumika kuwapa baadhi ya waamuzi ndio umekuwa na changamoto kubwa msimu huu.

Kundi kubwa la waamuzi hao, wanadaiwa kuwa wamepata fursa ya kuchezesha Ligi Kuu huku wakiwa hawana uzoefu wa kuchezesha kwa muda wa kutosha, mechi za ligi za madaraja ya chini kama vile zile za mabingwa wa mikoa, Ligi Daraja la Pili na Ligi Daraja la Kwanza.

Kutokana na kukosa uzoefu, presha ya kuchezesha mechi za Ligi Kuu hasa zile zinazohusu timu zenye majina makubwa au mashabiki wengi, imewafanya kuwa na hofu inayowalazimisha kufanya makosa katika uamuzi.

Kwa kawaida, refa wa kuchezesha Ligi Kuu anapaswa angalau awe amechezesha Ligi Daraja la Kwanza kwa takribani miaka minne au mitano lakini kwa msimu huu, wapo waamuzi ambao wamechezesha ligi hiyo baada ya kuchezesha kwa muda mfupi ligi za chini na wengine ndio kwanza wakiwa wanaingia katika fani hiyo.

Uthibitisho wa dhana ya refa kutakiwa kuchezesha ligi za chini kwa muda mrefu kabla ya kupanda Ligi Kuu, upo kwa mwamuzi mstaafu wa kimataifa wa Tanzania, ambaye kwa sasa ni Mkufunzi wa Kimataifa wa waamuzi anayetambulika na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Israel Nkongo.

Huyu alilazimika kuchezesha ligi za chini kwa muda wa miaka 10 kutoka 1994 hadi 2004 ambao, ndio mwaka alioanza rasmi kuchezesha Ligi Kuu.

Kukosa mazoezi ya kutosha

Uchunguzi wa gazeti hili pia umebaini kwamba, idadi kubwa ya waamuzi wamekuwa hawafanyi mazoezi ya mara kwa mara yale ya nadharia na pia ya vitendo hasa wale wa mikoani.

Waamuzi wengi wamekuwa wakifanya mazoezi hasa kabla ya kuanza kwa msimu pale wanapokuwa katika mchujo na baada ya hapo huwa hawapati fursa hiyo.

Lakini, pia wamekuwa hawapati fursa ya kukutana mara kwa mara kufanya marejeo ya uchezeshaji wao na kupigwa msasa wa mabadiliko ya mara kwa mara ya vipengele vya sheria 17 za soka jambo ambalo litawafanya wawe na uelewa mpana wa kuzitafsiri.

Hii hupelekea wakose utimamu wa miili jambo linalowafanya washindwe kuyaona na kutafsiri matukio mbalimbali kwa haraka, lakini pia hata kukosa uzoefu hali ambayo huwafanya wababaike kunapotokea tukio linalohitaji kutolewa uamuzi wa haraka.

Nidhamu ya woga

Wapo baadhi ya waamuzi ambao inadaiwa wamepata fursa ya kuchezesha mechi za Ligi Kuu kutokana na mahusiano yao na baadhi ya vigogo wa Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB) au Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na sio kutokana na uwezo wao.

Kutokana na hilo, waamuzi hao wanatajwa kuwa hulazimika kufuata maelekezo kutoka kwa wale ambao, wamewasaidia kupata fursa hiyo kwa kuzibeba timu ambazo wamekuwa na maslahi nazo.

Manufaa ambayo vigogo hao hupata ama huwa ni ya kifedha wanayopata kutoka kwa waamuzi, kirafiki ama maeneo ambayo wanatokea au yale ya timu wanazoshabikia kupata ushindi.

Mwaamuzi mwingine amefichua kuwa, kwa sasa wanapangwa kuchezesha mechi kutokana na ukaribu wa mikoa ambayo wanatoka kama anatokea Dar es Salaam basi atachezesha mechi za mkoa huu au iliyokuwa karibu.

“Kama mwamuzi anatokea Kanda ya Ziwa basi atapangiwa kuchezesha ni zile ambazo zinazunguka mikoa hiyo ya Kagera, Mwanza, Shinyanga na mingine ya jirani, lakini tofauti na hapo ni ngumu kupewa mechi za mbali.

“Nashindwa kuelewa mapungufu mengi ya waamuzi wenzangu yanatokea katika mechi nyingi ila kuna timu moja ndio yamekuwa mengi hasa kwenye Uwanja wa Taifa…sielewi kabisa hilo.

“Waamuzi tumekuwa na makundi yetu ya mitandao ya kijamii ambayo tupo wenyewe tumekuwa tukisemana na kupeana maneno makali kwa makosa haya kwani, hatuyapendi yafanyike.

“Imefikia hatua ya kukasirikiana wenyewe kwa wenyewe kutokana na matukio haya ambayo yanatuharibia muonekano wetu, lakini hili linaweza kuchangiwa au kutojua kutafsiri sheria,” anasema.

Bosi Bodi ya Ligi

Wakati waamuzi wakifichua kuwa wamekuwa wakikopwa kwa kutolipwa kwa wakati, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto amekiri kuwepo kwa tatizo la posho.

Hata hivyo, amesema kuwa kabla ya kupanga kazi hukubaliana na waamuzi na kuweka sawa baadhi ya mambo.

“Kabla ya kufanya kazi na waamuzi tunakubaliana mambo kadhaa kama anapokwenda kuchezesha mechi, atapata usafiri, mahali kwa kulala, chakula na posho.

“Sasa kuna kipindi hali inapokuwa mbaya kabla ya kumpanga mwamuzi kwenye mchezo husika, unamwambia hali halisi kuwa tutahakikisha unapata mahitaji yote muhimu isipokuwa posho tutakulipa mambo yakiwa mazuri. Tunakubaliana sasa kwa mtu, ambaye anaona mambo magumu haki yake kukataa asipangiwe mechi.

“Mwamuzi anapoamua kwenda kinyume na sheria za mchezo wa soka moja kwa moja anafanya kosa na ataadhibiwa hakuna sababu yoyote juu ya hilo. Kucheleweshewa posho sio sababu katika kazi yetu.

“Kazi ya waamuzi ni kujitolea na anayefanya hivyo anayekwenda kinyume na maadili ni kwamba hatufai. Moja kwa moja tunamchukulia kuwa ameingia kwenye kazi hii kwa sababu ya maslahi yake binafsi,” alisema Mnguto.

KARIA, MWAKYEMBE

Kwa upande wake, Rais wa TFF, Wallace Karia amesema kuwa tatizo la waamuzi ni kubwa kwa sasa na kwamba, hawezi kuwachukulia hatua wenyewe, lakini atapambana na watu waliopewa jukumu la kuwachukulia hatua.

Alisema TFF imezipa mamlaka Kamati ya Waamuzi na ile ya Uendeshaji kuhakikisha wanasimamia kikamilifu masuala yote kuhusu waamuzi na ligi, lakini kama watashindwa, basi ataingilia kati.

Juzi, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe aliliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuingilia kati malalamiko ya muda mrefu ya wadau wa soka kuhusu waamuzi kutoa uamuzi usio sahihi na unaolalamikiwa na wadau wengi wa mchezo huo.

Hata hivyo, TFF iliziagiza kamati za Waamuzi na Mashindano kukutana haraka jana kujadili tatizo hilo ambalo limelitia doa soka la Tanzania kwa sasa.

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...