Search This Blog

Wednesday, February 26, 2020

Hawakuachi ukiwachezea mipira ya juu Ligi Kuu England wanakuchapa

LONDON, ENGLAND . MABAO ya kila aina yamefungwa katika Ligi Kuu England msimu huu wa 2019-20, yapo yaliyotokana na juhudi binafsi, yaliomaliziwa kiulaini, mashuti makali na yale ya kichwa.

Wakati mashabiki wengi wakivutiwa zaidi na mabao ya mashuti makali na juhudi binafsi, watu wamekuwa wakiyachukulia poa mabao ya kichwa licha ya ukweli mengine hufungwa kwa uwezo wa hali ya juu.

Zipo aina nyingi za mabao ya kichwa, kuna yale yanayotokana na kichwa cha nguvu, cha kudundisha au kile kilichopigwa kwa ustadi wa hali ya juu na kumchagua kipa.

Msimu huu imechukua muda mrefu kidogo kwa timu zote 20 za Ligi Kuu kufunga bao la kichwa, Aston Villa ndiyo ilikuwa timu ya mwisho kufunga bao la kichwa msimu huu, ilifanya hivyo mwanzoni mwa Februari mfungaji likifungwa na Mtanzania Mbwana Samatta. Lakini, je, ni timu gani ndiyo inatisha zaidi kwa mabao ya vichwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu?

20. West Ham United

Mabao ya kichwa: 1

Advertisement

Mfungaji bora

(mabao ya kichwa):

Issa Diop (1)

Wastani katika mabao yote:

Asilimia 3.33

Moja kati ya timu tatu ambazo zimefunga bao moja tu la kichwa ni West Ham wakifanya hivyo katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Everton, mfungaji akiwa Issa Diop, Januari.

Timu hii imeshuka sana kwenye idara hii, msimu uliopita walifunga mabao 10 ya vichwa na inaonekana ubutu wao kwenye idara hii unawatesa.

19. Watford

Mfungaji Bora:

Troy Deeney (1)

Wastani katika mabao yote:

Asilimia 4.17

Timu nyingine inayopambana kukwepa kushuka daraja ambayo msimu huu imefunga bao moja tu la kichwa. Bao hilo ililifunga karibuni walipopigwa mabao 2-1 na Aston Villa, Januari. Troy Deeney ndiye alifunga bao hilo, Deeney msimu uliopita alifunga mabao ya aina hiyo matatu.

18. Norwich City

Mfungaji Bora: Kenny McLean (1)

Wastani katika mabao yote:

Asilimia 4.17

Inahitimisha hat-trick ya timu tatu zilizonafasi tatu za chini kwenye msimamo ambazo zote zimefunga bao moja tu la kichwa msimu huu, bao pekee la kichwa la Norwich lilifungwa Septemba wakati Kenny McLean alipofunga bao la kuongoza siku wakiipiga Manchester City kwa mabao 3-2.

Watford watakuwa wanaombea kupata matokeo ya aina hii kati ya sasa na mwisho wa msimu ili wabaki Ligi Kuu.

17. Aston Villa

Mfungaji Bora: Bjorn Engels, Mbwana

Samatta (1)

Wastani katika mabao yote: Asilimia 5.88

Aston Villa ndiyo ilikuwa timu ya mwisho ya Ligi Kuu England kupata bao la kichwa msimu huu, walifanya hivyo kupitia kwa Mbwana Samatta, Februari 1. Lakini hawakukaa muda mrefu wakata bao lingine kupitia kwa Bjorn Engels katika pambano dhidi ya Tottenham Hotspur.

16. Sheffield United

Mfungaji Bora:

Oliver McBurnie,

Enda Stevens (1)

Wastani katika mabao yote: Asilimia 7.14

Sheffield United imewashangaza wengi kwa kiwango chake msimu huu, sasa hivi wanapambana kutafuta nafasi ya kushiriki michuano ya Ulaya. Licha ya kiwango chao hawana makali sana kwenye idara ya mabao ya kichwa kwa sababu ni mabao mawili tu msimu huu wamefunga kwa kichwa kupitia kwa Oliver McBurnie na Enda Stevens.

15. Southampton

Mfungaji bora:

Wachezaji watatu (1)

Wastani katika mabao yote: Asilimia 9.38

Licha ya Danny Ings kufunga mabao mengi msimu huu, akifunga mabao 15 kati ya 32 yalifungwa na timu nzima, hajafunga bao hata moja la kichwa. Wachezaji waliofunga mabao ya vichwa ya Southampton ni Shane Long na mabeki wa kati Jack Stephens na Jannick Vestergaard.

14. Bournemouth

Mfungaji bora:

Wachezaji watatu (1)

Wastani katika mabao yote: Asilimia 11.54

Katika mapambano yao ya kutaka kubaki Ligi Kuu England, Bournemouth hawana makali sana mbele ya goli, wanakosa kiwango cha Callum Wilson. Amefunga bao moja kati ya mabao yao matatu ya kichwa msimu huu, lakini kwa jumla amefunga mabao saba tu.

13. Crystal Palace

Mfungaji bora:

Wachezaji watatu (1)

Wastani katika mabao yote: Asilimia 13.04

Crystal Palace ndiyo imefunga mabao machache zaidi katika Ligi Kuu England msimu huu. Hii inamaanisha hata mabao ya aina nyingine yamekuwa adimu, lakini moja kati ya mabao yao ya kichwa limefungwa na Cenk Tosun, aliyetua kwenye timu hiyo wakati wa Januari kwa mkopo akitokea Everton.

12. Arsenal

Mfungaji bora:

Pierre-Emerick

Aubameyang (2)

Wastani katika mabao yote: Asilimia 11.11

Pierre-Emerick Aubameyang anaongoza orodha ya ufungaji wa Ligi Kuu England hadi sasa akiwa na mabao 17, huku mabao mawili kati ya hayo akifunga kwa kichwa, Arsenal kwa jumla msimu huu wamefunga mabao manne tu ya kichwa wafungaji wengine ni David Luiz na Alexandre Lacazette.

11. Tottenham Hotspur

Mfungaji bora:

Harry Kane (2)

Wastani katika mabao yote: Asilimia 11.63

Msimu huu Tottenham imefunga mabao matano ya kichwa, mawili kati ya hayo yamewekwa kimiani na Harry Kane. Lakini wakati huu ambao Kane ni majeruhi wanakosa watu ambao ni wazuri kwenye mipira ya juu, msimu uliopita walifunga mabao 14 ya kichwa wakashika nafasi ya pili kwa aina hii ya mabao.

10. Manchester United

Mfungaji bora:

Anthony Martial (2)

Wastani katika mabao yote: Asilimia 13.16

Kabla ya kuichapa Chelsea, Jumatatu iliyopita, Manchester United ilikuwa imefunga mabao matatu tu ya kichwa, lakini mabao ya Anthony Martial na Harry Maguire yalipandisha idadi hiyo kufikia tano.

9. Wolverhampton

Mfungaji bora:

Raul Jimenez (3)

Wastani katika mabao yote: Asilimia 14.29

Wakicheza soka la kasi na kushambulia kwa kushtukiza Wolves si timu ambayo unaitarajia itafunga mabao mengi sana ya kichwa – wanapenda kupiga krosi za chini chini. Hatahivyo wamefanikiwa kufunga mabao matano huku Raul Jimenez akifunga mabao matatu.

8. Brighton and Hove

Mfungaji bora: Neal

Maupay, Adam Webster (2)

Wastani katika mabao

yote: Asilimia 19.35

Katika msimu ya karibuni Brighton imejitengenezea jina kama timu bora sana kwenye mipira ya kichwa, wakiwa na mtu kama Lewis Dunk katika kikosi chao. Hata hivyo msimu huu wamefunga mabao sita tu ya kichwa huku Neal Maupay na Adam Webster wakifunga mawili kila mmoja na Dunk moja.

7. Burnley

Mfungaji bora:

Chris Wood (5)

Wastani katika mabao

yote: Asilimia 20

Chris Wood ndiye baba lao kwenye idara hii, amefunga mabao mengi zaidi ya kichwa kuliko mchezaji yoyote katika Ligi Kuu England. Mabao matano. Ukiangalia staili yao ya uchezaji utashangaa kwa nini Burnley nzima imefanikiwa kufunga bao moja tu la ziada kupitia kwa Jay Rodriguez.

6. Leicester City

Mfungaji bora:

Jamie Vardy (3)

Wastani katika mabao

yote: Asilimia 12.96

Leicester wanakaribia kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na wanastahili hiyo nafasi. Timu hiyo imekuwa hatari sana mbele ya goli, wakifunga mabao saba ya vichwa huyo Jamie Vardy akiwa na mabao matatu ya kichwa.

5. Chelsea

Mfungaji bora:

Tammy Abraham (3)

Wastani katika mabao

yote: Asilimia 16.28

Chelsea kuna wakati imekuwa ikipata wakati mgumu kufunga, lakini hata hivyo msimu huu imefunga mabao saba ya kichwa. Ni wachezaji watatu tu ndiyo wamefunga mabao hayo Tammy Abraham akifunga matatu Christian Pulisic na Antonio Rudiger, wakifunga mawili kila mmoja.

4. Newcastle United

Mfungaji bora:

Wachezaji saba (1)

Wastani katika mabao

yote: Asilimia 29.17

Japokuwa Newcastle imefunga mabao saba ya kichwa msimu huu, lakini hakuna mchezaji hata mmoja aliyefunga mara mbili. Timu hiyo imekuwa ikipondwa kwa kushindwa kutumia mipira iliyokufa mabeki wanne wamefunga mabao ya kichwa. Cha kushangaza zaidi ni kuwa Andy Carroll hana bao hata moja la kichwa.

3. Manchester City

Mfungaji bora: (headers): Sergio Aguero,

Gabriel Jesus (2)

Wastani katika mabao

yote: Asilimia 11.94

Manchester City ndiyo timu yenye mabao mengi zaidi msimu huu, lakini ni mabao yao nane tu ndiyo yamefungwa kwa kichwa kutokana na mipira iliyokufa. Kinachofurahisha hapa ni kuiona Man City ikiwa juu kwenye idara hii licha ya aina ya soka lao la pasi fupi fupi. Licha ya vimo vyao Sergio Aguero na Gabriel Jesus, ndiyo wamefunga mabao mawili mawili ya kichwa msimu huu.

2. Everton

Mfungaji bora: Dominic Calvert-Lewin (4)

Wastani katika mabao

yote: Asilimia 32.35

Moja kati ya timu mbili kufunga mabao zaidi ya 10 msimu huu kwa kichwam Everton imekuwa bora sana kwa mipira ya juu, Dominic Calvert-Lewin ndiyo muuaji wa timu hiyo akiwa amefunga mabao manne ya vichwa kati ya 11 msimu huu.

1. Liverpool

Mfungaji bora: Virgil

van Dijk (4)

Wastani katika mabao

yote: Asilimia 21.31

Ipo kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England, kilele cha timu zenye mabao mengi ya kichwa, Liverpool wamethibitisha wanaweza kufanya kila kitu msimu huu. wakiwa na wachezaji kama Trent Alexander-Arnold na Andrew Robertson wakipiga krosi za hatari kila siku na jitu la miraba minne kama Virgil van Dijk ambalo limefunga mabao manne si ajabu kuona wakiwa juu kwenye orodha hii.

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...