
KITAA bei ya nyanya haikamatiki, lakini kweli ndio bei yake uifananishe na CD za Bongo Movie? Ni ubishi usio na refa kati ya Luqman Maloto na Dk Levy. Upo mjadala wa staa wa Yanga, Morrison kucheza rafu mbele ya mwamuzi bila kuadhibiwa.
LUQMAN: Pokea salamu kutoka kwangu yenye ladha ya kiwiko cha Morrison mbele ya refa na kadi hakupewa. Salamu ya pili ni penalti ya maajabu, mchezaji kadondoshwa mstarini refa kaweka faulo, lineman akasema penalti. Salamu ya tatu ni kwa penalti ya kuangulia maembe Kibada ambayo Morrison aliipiga. Salamu ya nne ni kwa ajili ya kukufariji wewe Yanga lialia. Timu itakutoa kamasi shauri yako.
DK LEVY: Unakumbuka kutoa salamu tu. Utadhani enzi za kina Chesco Mzee wa Matunda pale Sinza Afrika Sana. Ila ubishi wako juu ya kiwango cha Rich Mavoko kushuka baada ya kujitoa WCB unajisahaulisha. Tatizo lenu wewe na wanaomzunguka Richard na yeye mwenyewe mlishaona yeye na Mondi wako sawa. Nilikuambia Mavoko alikuwa bado sana kujenga himaya yake. Hata alipokuwepo watu waliona baada ya Mondi ni Jeshi Konde Boy kisha nafasi ya tatu washindanie Mavoko na Rayvanny. Kuwepo kwake WCB kulikuwa na nafuu kuliko hivi sasa yaani anazunguka kama inzi kwenye chupa. Alitakiwa akaushe kwanza atengeneza msitu wa fans kama Jeshii.
LUQMAN: Unapungukiwa taarifa halafu una ugonjwa wa kusahau. Mavoko alipokuwa WCB ulimnanga sana Harmonize kuwa anamuiga Diamond. Leo unajiita Konde Gang, halafu unamshambulia Mavoko. Isije ikawa baadaye yule Mavoko alitafuna mbivu zako ndio maana unamchukia, vijana hawana adabu wale. Si unajua Mavoko ana pesa ndefu? Handsome fupi, lebo yake inaitwa Billionaire Kid. Utamuweza? Huyo Harmonize wako pumzi imekata. Nenda YouTube ukaone anavyogalagazwa na Rayvanny.
DK LEVY: Toa mboyoyo zako. Hata East Coast Team, AY na FA walijiengua kwa sababu wao walikuwa na soko bila kutegemea kale kakundi mbinuko kalikoundwa na mabitoz na masela wachache. Ndivyo ilivyo kwa Prof. Jay na Hard Blasters. Jay alifikia wakati akawa mkubwa kuliko kundi. Kuamua kufanya kazi kivyake alikuwa sahihi. Unadhani Ngwea alifanya kazi binafsi kindezi nje ya Chamber Squard? Au Ferouz na Daz Nundaz? Ni kwa kuwa walikuwa juu ya hivyo vikoba vyao vya muziki.
LUQMAN: Haya sasa, Mavoko ameshaondoka WCB, wewe kinachokuuma ni kitu gani? Na sasa hivi anapiga hela kuliko alivyokuwa WCB. Msikitikie Harmonize wako anayeburuzwa YouTube na Rayvanny.
DK LEVY: Watu wabishi sampuli yako wapo kitambo. Ndo kina Tomaso wale wa Uyunani. Wewe ndo kina walewale wa kizazi hiki. Endelea kubishana na ukweli. Mavoko alidhani naye ni Christian Bella mbele ya Akudo Impact? Pia kumbuka unaweza kuwa mkali lakini huwezi kusonga bila kusimamiwa. Hilo lilimshinda Banza Stone, Choki, Muumini na TX Moshi William. Walikuwa na uwezo na mashabiki wengi lakini waliishia kuwa chini ya watu. Uwezo ni moja na kujisimamia ni jambo lingine tofauti na zito. Kuna wengine ndo tatizo zaidi, hawawezi kujisimamia wala kusimamiwa. Kama Wema Sepetu, Chid Benz, TID na Chilla.
LUQMAN: Kati ya binadamu wa kuwashangaa zaidi muongo huu ni wewe. Nimeshakwambia mambo ya Mavoko achana nayo. Wewe nenda YouTube ukamsaidie Konde Gang.
DK LEVY: Endelea kunishangaa badala ya Nyoshi El Sadat. Ambaye yupo nchini tangu miaka ya 80 lakini Kiswahili hajui kuongea. Kusema “ndio vile” yeye anasema “njo vile”. Mtu wa watu yeye anasema “mutu ya watu”. Kichekesho ni kwamba wapo Wabongo wanahusudu kuongea hivyo ili wajione kama Wakongo. Kipimo cha akili mbovu ni kitendo cha Mtanzania kutamani Ukongomani. Papaa Zahera anazurura tu mjini hapa akiutamani Utanzania, kisha Rajab wa Mbagala Kibonde Maji anatamani Ukongo. Halafu mchongo mkubwa wa Wakongo ni kulelewa na mashangingi skrepa ya Kino, Makumbusho na Mwananyamala huko. Kifupi hawana issue mjini.
LUQMAN: Ulivyo mzinguaji, unakimbilia kujificha kwa Nyoshi, kiwiko na penalti ya Morrison umekwepa. Unapenda sana mambo yasiyokuhusu. Yenye kuihusu Yanga yako na Morrison wako unakwepa.
DK LEVY: Achana na stori za fundi wa mpira Morrison. Kile kiwiko alichomtwanga yule mjelamjela, ilikuwa sawa tu. Timu inatoka Ruanda Nzovwe huko Mbeya baridi kama lote. Inasafiri kilometa zaidi ya 800 kuja Daslama mjini kumkaba mtu mmoja tu? Wangetumia nguvu hizo kukaba wengine leo wangekuwa mabingwa kabla ligi haijaisha. Kwanza ongelea dada zetu Twiga Stars huko wanawatandika tu wenzao. Haya mambo ya kusubiri Yanga kubeba ndoo msimu huu ni sawa na kusubiri ndoa ya Lulu na Majizo. Wakati suala la ndoa ni mipango ya Mungu Baba Mwenyezi. Suala la ubingwa kwa Yanga ni mipango ya Nabii Tito na Mchungaji Mashimo.
LUQMAN: Kwa hiyo umeikatia tamaa Yanga yako? Ikipindua matokeo na kuchukua kombe, wewe hutashangilia?
DK LEVY: Unauliza swali gani hilo? Yanga hawawezi kubeba ubingwa msimu huu. Mara ya kwanza kosa lilikuwa ni marefa kupendelea wengine. Baadaye ikawa suala la kusahaulika kwenye ratiba. Unategemea mtu kubeba ndoo hapo? Usisahau fitna za kipensi cha Zahera. Sasa wapinzani wanatumia nguvu za giza kusaidia timu zinazokutana na Yanga. Na zaidi vitimu vya mikoani vinatumika kiibilisi kutaka kumuumiza Morrison ili asikutane na wale watumishi hewa wa Msimbazi. Nakujibu kabla hujauliza maana lazima utauliza. Kagere, Bocco, Wawa na Nyoni wote hao ni watumishi hewa. Muda wao wa kustaafu ushapita sana. Wanaendekeza njaa tu.
LUQMAN: Acha kumsifia mchezaji wako wa freestyle. Huyo Morrison na maonesho yake ya mpira, huoni kama anaweza kuongeza udambwidambwi Bongo Movie na kupanua soko? Jibu kama mtu aliyezaliwa timamu, sio ulete majibu takataka hapa.
DK LEVY: Kuhusu suala la soko la sinema zetu siwezi kukupa jibu lolote. Au niseme sina jibu la moja kwa moja. Nitashauri tu. Hivi sasa nyanya soko lake liko juu sana. Nyanya moja bei kubwa kuliko CD ya Bongo Movie. Sasa kwa kuwa Serikali imehamia Dodoma. Bongo Movie nao wangefikiria tu michongo mingine. Tatizo nilikuwa mkali wa kuigiza enzi za kina Bishanga.
LUQMAN: Kwa taarifa yako Bongo Movie bado ipo poa. Ona tamthiliya zinavyopiga bao kila luninga kwa sasa. Wewe upo wapi?
DK LEVY: Wao wanahamia kwenye tamthiliya. Ni muda wa kubadili gia angani tu. Hakuna haja ya kushikilia jambo moja wakati jambo lenyewe halikutaki.
No comments:
Post a Comment