
Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta amesema kipaumbele cha kwanza baada ya kujiunga na Aston Villa ni kuinusuru na janga la kuteremka daraja.
Akizungumza jana, Samatta alisema atahakikisha anafunga idadi kubwa ya mabao katika mechi za Ligi Kuu England msimu huu.
“Niko tayari kucheza kwa kujituma kama kawaida yangu lengo ni kuhakikisha napeperusha bendera ya nchi yangu. Naamini hatuwezi kushuka daraja chukua kauli yangu,”alisema Samatta alipozungumza na gazeti hili.
Samatta alisema anatarajia kupata ushirikiano wa wachezaji wenzake wa Aston Villa ili kuivusha katika kipindi kigumu inachopitia msimu huu.
Aston Villa inayonolewa na kocha Dean Smith raia wa Uingereza ipo nafasi ya 18 kati ya timu 20 ikiwa na pointi 22 kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Watford.
Samatta alisema ndoto ya kujiunga na Aston Villa imetimia baada ya kuvutiwa na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Gabby Agbonlahor.
Alisema tangu akiwa mdogo alikuwa akivutiwa na Mnigeria Agbonlahor aliyekuwa kinara wa mabao katika kikosi hicho. “Najua mambo mengi kuhusu Aston Villa lakini moja ni wachezaji waliokuwa wakicheza hapa siku za nyuma kama Gabby Agbonlahor,” alisema Samatta.
Muda mfupi baada ya Samatta kutambulishwa rasmi, kocha wa Aston Villa Dean Smith alisema alikuwa na ndoto ya kumsajili mshambuliaji huyo.
Smith alisema ana matumaini Samatta atainusuru Aston Villa na janga la kuteremka daraja baada ya kufanya vibaya katika mechi za Ligi Kuu msimu huu.
“Nina furaha kumpata Mbwana Samatta ni mfungaji hodari wa muda wote ambaye nimemfahamu, nitafanya naye kazi vizuri,”anasema Smith.
Kocha huyo alisema Samatta ni mfungaji bora na matumaini yake ni kumuona akiendeleza moto wake. Samatta ni mchezaji wa tatu kutua Villa Park akitanguliwa na Danny Drinkwater (Chelsea) na Pepe Reina (AC Milan) waliotua kwa mkopo.
Wakizungumza jana, kocha Kenny Mwaisabula alisema Samatta alikuwa na juhudi binafsi uwanjani tangu akiwa mdogo alipokuwa mchezaji wa timu ya Temeke. “Nilikuwa mwalimu wake timu ya Mkoa wa Temeke alikuwa kijana mdogo lakini alikuwa akipambana na Rashid Gumbo na wengine,”alisema Mwaisabula.
“Nafasi ya Samatta kucheza ipo anatakiwa kuitumia vizuri nafasi hii kuendeleza mazuri aliyofanya akiwa Genk,” alisema mchambuzi Ally Mayay.
Mshambuliaji wa zamani wa Simba Zamoyoni Mogella amewataka wachezaji wa hapa nchini kuiga mfano wa Samatta kwa kuzingatia nidhamu ndani na nje ya uwanja.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk Harrison Mwakyembe alitoa pongezi kwa Samatta kujiunga na Aston Villa. Pia Chadema ilitoa taarifa ya kumpongeza kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu England.
No comments:
Post a Comment