Search This Blog

Saturday, January 25, 2020

Maafisa Michezo wa Mikoa na Halmashauri waagizwa kubadilika kiutendaji

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe amewaagiza maafisa michezo wote chini kubadilika katika utendaji wao kutokana na kulalamikiwa na wadau wengi wa michezo namna ambavyo wanashughulikia sekta hiyo

Waziri Mwakyembe ametoa agizo hilo jana Jijini Arusha alipokutana na wadau wa michezo kujadili maendeleo ya sekta hiyo ambapo amewataka maafisa michezo kuhakikisha masuala ya michezo katika maeneo yao hayakwami kutokana na wao kutowajibika.

“Nyinyi ni watumishi wa Serikali mnaposhindwa kutatua kero za wanamichezo na kusimamia sekta hii basi nyie hamtoshi na mimi sitawavumilia kuona mnakwamisha maendeleo ya michezo nchini”alisema Dkt.Mwakyembe.

Aidha Mhe.Waziri ameliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ifikapo Februari mosi 2020,liwe limewasilisha mapendekezo ya mabadilio ya Katiba ya Chama cha Riadha nchini ili kupata muongozo wa mchezo huo.

Mhe.Waziri ameongeza kuwa Serikali imerudisha michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA ili kuhakikisha sekta hii inaendelea kukua na kuletea heshima taifa, huku akieleza kuwa Serikali inadhamiria kutofautisha viwanja vya sanaa na vya michezo kwasabu sekta hizi zina wadau wengi ambao wamekuwa na matukio yanayofanana na  yanayofanyika kwa wakati unaofanana hivyo ni vyema kila sekta ikajitegema katika maonyesho yake.

Vile vile Dkt.Mwakyembe amevitaka vilabu vya michezo na mashirikisho kuona umuhimu wa kutumia wanamichezo wa ndani ili kuinua vipaji walivyonavyo lakini pia kuwapatia ajira kuliko kusajili wachezaji wa nje wengi na kuwaacha wazalendo.

Kwa upande wake Afisa Michezo wa Mkoa Bibi  Mwamvita Okeng’o amesema kuwa Mkoa wa Arusha unaendelea kufanya vizuri katika michezo na unaendelea kukuza sekta hiyo kwa kuongeza idadi ya viwanja na tayari mipango imeanza ya kujenga uwanja kila Wilaya ya mkoa huo.

Katika hatua nyingine Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Riadha Bw.Wiliam Kalaghe amesema kuwa maandalizi ya wanamichezo Alphonce Simbu na Failuna Abdu ambao wataliwakilisha Taifa mwaka huu katika mashindano ya Olympiki  huko Japan yanaendelea vizuri na tayari shirikisho hilo limetoa kiasi cha Sh. Milioni 03 kama chagizo la maandalizi hivyo watanzania wanapaswa kuwaunga mkono.

Naye Bw.Hamis mdau wa mchezo wa mpira wa miguu ameshauri wanamichezo kujifunza lugha na namna bora ya kufanya mahojiano ili wanapokuwa wamepata nafasi ya kucheza soka nje wasikwame kwa kigezo cha kushindwa kujibu maswali au kutumia lugha Fulani.

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...