Search This Blog

Tuesday, January 28, 2020

By Edo Kumwembe

Bernard Morrison, winga wa kimataifa wa Ghana anawasisimua Wanayanga. Anaupanda mpira anavyojisikia. Yanga wakishinda anaanza kufanya mambo yake. Anaupanda mpira kwa juu anauburuza, mashabiki wa Yanga wanakenua meno kwa furaha.

Yanga hawapitii nyakati nzuri sana kwa sasa. Lakini wanapopata kibwanga kizuri wanatumia fursa hiyo kuwanyima raha wapinzani wao Simba. Na kweli, Morrison anawanyima raha kwelikweli Simba kwa sababu Yanga wanapiga kelele zinazopitiliza.

Mechi mbili zimepita na Yanga wameshinda mabao matano kwa moja. Walishinda 3-1 kule Singida na wameshinda mabao 2-0 juzi Jumapili dhidi ya Tanzania Prisons katika michuano ya Kombe la FA. Juu ya yote Morrison anacheza huku ‘akitembea juu ya mpira’.

Hii staili yake inaitwa Shibobo. Asili yake kubwa ni Afrika Kusini. Waafrika Kusini wanapenda staili hii. Kuanzia wachezaji hadi mashabiki. Baada ya ushindi wanataka mtu ambaye anaurukauruka mpira na kuuchezea katika mbwembwe zisizo na maana.

Pale Afrika Kusini wataalamu wa Shibobo ni pamoja na Thabo Rakhale, Masibusane Zongo, Mark Mayambela, Fortuna Makaringe, Thabo Mooki, Jabu ‘Pule” Mahlangu na wengineo. Wakiongoza 2-0 aun 3-0 na mpira ukifika dakika ya 75 wanaanza Shibobo zao.

Hata Morrison juzi nilimuona akianza Shibobo zake katika dakika ya 74 baada ya Yanga kuongoza kwa mabao 2-0. Huu ndio utaratibu wa Shibobo. Kama timu inaongoza 1-0 wachezaji huwa hawafanyi Shibobo. Ni rahisi kwa adui kurudisha akanyamazisha Shibobo.

Advertisement

Morrison anatoka Afrika Magharibi na upande ule huwa hawana mambo haya. Upande huo unatuzalishia watu wengi wa kazi ambao wanaenda kutamba Ulaya. Hawana muda wa kupiga Shibobo kwa sababu makocha wa Kizungu hawataki.

Morrison inaonekana alijifunzia mambo haya Afrika Kusini. Yamemkaa katika mwili.

Na sasa amefika nyumbani kwake. Kwanini? Mashabiki wa Yanga watampenda. Ni mchezaji mzuri kwa ajili ya kuumiza roho za mashabiki wa timu pinzani wakati Yanga inaongoza.

Mashabiki wa Tanzania hawana tofauti sana na wale wa mashabiki wa Afrika Kusini. Wote ndio maana hawana wachezaji wengi wa kulipwa barani Ulaya. Mashabiki wa pande zote hizi mbili bado wamebakia katika mpira wa mbwembwe (skills) kuliko mpira wa mbinu (tactics).

Kwa hizi Shibobo, Morrison amefika katika nchi yake. Ili mradi tu Yanga iongoze mechi. Wakati mwingine anaweza kuzifanya hata wakati Yanga inaongoza kwa bao moja. Anazifanya na anashangiliwa, kwanini aache? Amefika katika nchi ambayo watu wanapenda kanzu kuliko pasi murua ya mwisho inayozaa bao.

Kitu kizuri kuhusu Morrison ni kwamba anafanya Shibobo zake baada ya kufanya mambo fulani ya msingi uwanjani. Kwa mfano, pale Singida alishapiga pasi nzuri kwenda kwa Haruna Niyonzima kisha akafunga. Juzi alifunga bao la penalti na kupika bao la pili kwa Yanga.

Kitu kingine kizuri kuhusu Morrison na Shibobo zake ni kwamba atakuwa anasababisha faulo nyingi kuelekea kwa wapinzani. Kuna mabeki kama kina Juma Nyosso hawatakubali ‘ujinga huu’. Watashikwa na jazba nyingi ambazo zitapelekea wamchezee rafu za kijinga.

Kule Afrika Kusini kama unacheza Shibobo na hauna madhara wachezaji wa timu pinzani wanakutazama tu. Hapa Bongo naweza kuhisi kile ambacho kimekaa katika moyo wa Nyosso na washikaji zake kabla ya pambano la marudiano kule Kagera. Tusubiri.

Kitu kingine kuhusu Shibobo za Morrison ni kwamba ataimuibua Haruna Niyonzima. Namjua Haruna. Hatakubali kufunikwa na kivuli cha Shibobo. Yeye ndiye aliyekuwa mfalme wa Shibobo kabla ya kutua kwa Morrison pale Jangwani, ingawa alikuwa haupandi mpira juu.

Haruna atarudisha Shibobo zake kwa kasi. Lakini atajitahidi pia kufanya mambo muhimu ili mradi Yanga waburudike na kipaji chake maridhawa. Sasa kutakuwa na mashindano ya Shibobo kati ya Haruna na Morrison.

Kitu kitakachowakanganya Yanga ni kwamba kocha yeyote Mzungu mwenye akili timamu hawezi kukubali Shibobo. Nimesikia Kocha wa Yanga, Luc Eymel akiwashangaa mashabiki wa Yanga kwa kumshangilia Morrison na Shibobo zake.

Ugomvi utakuja pale ambapo atakapokuwa anapiga Shibobo nyingi na kisha kutolewa uwanjani kwa hasira za kocha. Mashabiki hawatamuelewa kocha Mzungu. Nasubiri kwa hamu kuona ambacho kitatokea.

Vipi kuhusu waamuzi? Watapata wakati mgumu. Itabidi warudi nyuma na kusoma vitabu vyao vema. Kule Afrika Kusini, ukizidisha sana Shibobo unapewa kadi ya njano. Kikanuni inatajwa kwamba ‘unaamsha hasira za wapinzani’.

Kama unafanya Shibobo kwa haraka haraka kama alivyofanya Morrison na kisha kupiga pasi basi mwamuzi anaruhusu mpira uendelee. Kama hautaki kuwaachia mpaka unapiga magoti, basi unapewa kadi ya njano kwa kuuhatarisha mchezo wenyewe na kuwatia wapinzani katika hasira.

Ulaya hawapendi mambo haya. Ni Afrika na Amerika Kusini ndipo kuna michezo hii ‘ya kijinga’. Walimu wa Ulaya wanapenda mchezo uende kasi na timu yake iendelee kushindilia mabao kwa adui hata kama kuna tofauti ya mabao mawili au matatu.

Afrika na Amerika Kusini michezo hii ‘ya kijinga’ ni mingi kwa sababu mpira wetu tunaanzia barabarani, ufukweni na barazani. Tunakuja kufundishwa soka baadaye lakini kwanza tunaanzia katika vurugu za kila mtu kuonyesha uhodari wake binafsi. Hapa ndipo Shibobo zinapoanzia.

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...