Search This Blog

Tuesday, December 3, 2019

Wazawa tishio kwa wageni Ligi Kuu

By Olipa Assa, Charles Abel

Dar es Salaam. Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikisimama kwa muda kupisha mashindano ya Kombe la Chalenji, nyota ya wazawa wameonekana kufanya vyema kulinganisha na wageni katika raundi 13 zilizochezwa hadi sasa.

Tofauti na misimu ya nyuma ambayo wachezaji wa kigeni ndio walikuwa wakitamba kuanzia mwanzo hadi mwishoni mwa ligi, mambo yamekuwa tofauti msimu huu kutokana na kiwango bora cha wachezaji wazawa ambacho wamekuwa wakikionyesha katika timu zao.

Kasi ya kufumania nyavu ni eneo la kwanza ambalo nyota wazawa wameonekana kuwa moto wa kuotea mbali msimu huu kulinganisha na wale wa kigeni.

Ukimuondoa, Meddie Kagere wa Simba ambaye anaonekana kuwapa wakati mgumu wazawa katika vita ya kusaka zawadi ya ufungaji bora msimu huu, hakuna mchezaji mwingine wa kigeni ambaye ameonekana kuwa tishio dhidi ya wazawa katika kufumania nyavu jambo linalotoa ishara njema kuwa tatizo sugu la ubutu kwa washambuliaji wa Kitanzania linaanza kupata tiba.

Nyuma ya Kagere mwenye mabao manane, yupo Paul Nonga wa Lipuli anayemnyemelea kwa kasi akiwa na mabao saba na wanaofuatia ni wazawa Miraji Athuman (Simba) na Daruwesh Saliboko (Lipuli) ambao kila mmoja amefumania nyavu mara sita.

Katika kundi la wachezaji waliofunga mabao matano, hakuna mchezaji wa kigeni, wanaotamba hapo ni Yusuph Mhilu (Kagera Sugar) na Peter Mapunda wa Mbeya City.

Advertisement

Wageni wawili, David Molinga (Yanga) na Obrey Chirwa (Azam) wanakuja kuchomoza katika kundi la wachezaji waliopachika mabao manne kila mmoja wakiwa sambamba na idadi kubwa ya wachezaji wazawa ambao ni Gerard Mdamu (Mwadui), Samson Mbangula (Prisons), Awesu Awesu (Kagera Sugar) na Waziri Junior (Mbao FC).

Alipotakiwa kutoa maoni yake juu ya takwimu hizo, kocha Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ alisema kinachofanywa na wazawa ni ishara tosha kuwa wakiaminiwa wanaweza kufanya vizuri.

Eneo lingine ambalo wazawa wamekuwa hawana mzaha msimu huu ni katika vita ya namba. Wamekuwa wakipata nafasi ya kucheza mara kwa mara na kwa muda mrefu kulinganisha na wageni wengi.

Mfano wa hilo unajidhihirisha katika vikosi vya timu tatu za Simba, Yanga na Azam ambazo zimetumia bajeti kubwa ya usajili kuliko nyingine. Tofauti na msimu uliopita ambako wageni walikuwa wanaanza kwa idadi kubwa katika kikosi cha Yanga, mambo ni tofauti msimu huu kwani baadhi yao wamejikuta hawana namba za kudumu.

Ni wachezaji watano tu kati ya 10 wa kigeni wa Yanga ambao wana uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza ambao ni kipa Farouk Shikhalo, nahodha Papy Tshishimbi, Patrick Sibomana, David Molinga na Lamine Moro.

Maybin Kalengo, Issah Bigirimana, Seleman Mustafa na Juma Balinya wamekuwa wakisota benchi huku Sadney Urikhobi amekuwa hana uhakika wa nafasi ya kudumu kikosini.

Wageni sita kati ya 10 waliosajiliwa na Azam msimu huu, Richard Djodi, Donald Ngoma, Razack Abalora, Daniel Amoah, Selemani Ndikumana na Emmanuel Mvuyekure wamekuwa wakisugua benchi.

Simba ambayo msimu uliopita, kikosi chake kilikuwa na wastani wa kuchezesha nyota saba wa kigeni, safari hii wazawa ndio wamekuwa na umuhimu na mchango mkubwa wakipata sapoti ya wageni wachache.

Mabeki Tairone Santos na Pascal Wawa hakuna mwenye uhakika wa kuanza kikosini kama ilivyo kwa viungo Clatous Chama, Sharaf Shiboub, Francis Kahata na Gerson Fraga pamoja na mshambuliaji Wilker da Silva.

Prisons inaweza kuwa timu iliyoshtua zaidi kutokana na kutopoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu msimu huu hadi sasa, ikipata ushindi katika mechi nne na kutoka sare nane.

Hata hivyo, timu inayoongoza katika msimamo wa ligi na pia kwa kupachika mabao ni Simba ikiwa imefunga 19 lakini pia imeonekana kuwa na safu imara zaidi ya ulinzi ikiruhusu mabao matatu tu katika mechi 10 ilizocheza.

Raundi hizo 13 zimeonyesha kuongezeka kwa njaa ya kufumania nyavu kwa washambuliaji na ushahidi wa hilo ni kuongezeka kwa idadi ya wachezaji waliopachika mabao matatu katika mchezo mmoja ‘hat trick’ kutoka wawili msimu uliopita hadi watatu msimu huu.

Wachezaji hao ambao wamefunga mabao matatu katika mchezo mmoja msimu huu ni Paul Nonga, Obrey Chirwa na Ditram Nchimbi (Polisi Tanzania) wakati msimu uliopita, hadi raundi ya 13 ya Ligi, kulikuwa na wachezaji wawili tu waliopachika mabao matatu katika mchezo mmoja kwa nyakati tofauti ambao walikuwa ni Emmanuel Okwi (Simba) na Alex Kitenge (Stand United).

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wadau mbalimbali wa soka, wamesema ligi ya msimu huu imeonyesha ushindani na msisimko wa hali ya juu ingawa mabadiliko ya ratiba yanapunguza ladha yake.

“Timu zimeonyesha kupambana na kilichokuwa kinanifurahisha ni namna ambavyo unaona timu moja inakuwa na washambuliaji wanaoshindana kufunga mfano Simba kuna Kagere, Miraji na Lipuli, Nonga na Saliboko,” alisema kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Mohamed Mwameja.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Ally Tigana alisema kusimama kwa ligi kunaifanya isiwe bora na kupooza kwa ushindani ambao ulikuwepo.

Kocha wa zamani wa Stand United, Athuman Bilali ‘Bilo’ alisema timu zinaonekana zilijiandaa vya kutosha kabla ya kuanza kwa msimu.

“Soka la mvuto linachezwa, timu zinajitahidi kupata matokeo, kikubwa isisimame sana kwani itaondoa msisimko ambao ulikuwepo, kwani wachezaji wakikaa sana mapumziko wanajisahau,” alisema.

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...