
MANCHESTER, ENGLAND . MANCHESTER City wamekoleza moto wao kwenye mpango wa kumchukua Mauricio Pochettino kwenda kuwa kocha wao mpya kama Pep Guardiola atafungasha virago vyake kuondoka, licha ya Mhispaniola huyo kudai hana mpango wa kuachana na timu hiyo.
Guardiola mipango yake ya muda mrefu kwenye kikosi cha Man City imekuwa kwenye utata mkubwa kwa siku za karibuni baada ya kocha huyo kuhusishwa na mpango wa kuachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu.
Huu ni mwaka wake wa nne kwenye kikosi cha Man City huku rekodi za kocha huyo zikionyesha kwamba hajawahi kuinoa timu yoyote kwa miaka mitano. Man City kwa sasa wanahaha baada ya msaidizi wa Guardiola kwa miaka mitatu, Mikel Arteta, kukubali dili la kwenda kuinoa Arsenal, ambayo imemfukuza kazi kocha wake Unai Emery.
Arteta anataka kwenda kuwa kocha mkuu katika klabu yake ya zamani na hapo ametajwa kwamba huenda akamchukua kocha mwingine msaidizi wa Man City, Rodolfo Borrell kwenda naye wakapige mzigo huko Emirates.
Guardiola amekuwa akisisitiza kwamba hana mpango wa kuondoka Man City baada ya kusema: "Nipo freshi kabisa kufanya kazi na timu hii. Unapokuwa sehemu kwa miaka mitano inategemea na matokeo. Tutasubiri kuona kitakachotokea msimu huu na msimu ujao."
Lakini, wasiwasi wa kuondoka Arteta na Borrell unawafanya Man City kuwa kwenye hofu kubwa ya kocha wao huyo kama atabaki kwenye kibarua hicho na ndio maana sasa wanaanza kumtolea macho Pochettino, ambaye aliachana na Tottenham Hotspur hivi karibu.
No comments:
Post a Comment