Search This Blog

Monday, December 16, 2019

Kilimanjaro Stars kupenyea hapa Uganda

By Charles Abel

UDHAIFU wa walinzi wa Uganda katika kuwasiliana pamoja na ukabaji unaweza kuwa msaada kwa timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kupata ushindi kwenye mchezo wa nusu fainali leo Jumanne dhidi yao lakini ikiwa tu washambuliaji wa Stars watautumia vyema

Mabeki wa Uganda wamekuwa wakifanya makosa ya mara kwa mara ya kuwaruhusu washambuliaji wa timu pinzani kulifikia lango lao, makosa ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakichangiwa na mawasiliano duni na kutegeana baina yao.

Pamoja na timu hiyo kuonekana kuwa tishio katika mashindano ya Chalenji yanayoendelea, changamoto hiyo inaonekana kutofanyiwa kufanyiwa kazi na benchi lao la ufundi na huenda ikageuka neema kwa Stars pindi zitakapokutana katika nusu fainali ya pili itakayopigwa kwenye Uwanja wa KCCA kuanzia saa 10 jioni.

Awali ratiba ilionyesha kuwa timu hizo zingekutana katika mechi ya kwanza ambayo itachezwa saa 7.30 mchana lakini juzi usiku ilibadilishwa na kuiweka iwe ya pili ikitanguliwa na ile itakayozikutanisha Eritrea na Kenya.

Makosa hayo yanayojirudia kila wakati yameifanya Uganda kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi dhidi ya Burundi ambayo waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na mechi ya mwisho dhidi ya Djibout waliyopata ushindi wa mabao 4-1.

Lakini udhaifu huo ukionekana kuwa fursa inayoweza kutumiwa na Stars kuwamaliza Uganda, uimara na makali ya safu ya ushambuliaji na ile ya kiungo ya wenyeji unapaswa kuifanya Kilimanjaro Stars kuingia na tahadhari ya hali ya juu katika mechi ya leo.

Advertisement

Safu ya kiungo ya Uganda inayoongozwa na mkongwe Muzamiru Mutyaba huku ikiwa pia na kijana aliye katika kiwango bora kwa sasa Bright Anukani, imekuwa ikileta muunganiko mzuri wa kitimu ambao umekuwa ukiiwezesha Uganda kutawala mchezo, kutengeneza nafasi na kufunga idadi kubwa ya mabao kulinganisha na timu nyingine ambazo zimeshiriki mashindano haya.

Hadi inafika hatua ya nusu fainali, Uganda imepachika jumla ya mabao 10 katika mechi nne huku Anukani na Allan Okello kila mmoja akipachika mawili yanayowafanya wawe vinara katika mbio za kuwania ufungaji bora wa mashindano hayo.

Okello anayechezea KCCA ya Uganda, ni mchezaji wa safu ya ushambuliaji ya Uganda anayepaswa kuchungwa zaidi kutokana na ujanja wake wa kufumania nyavu, uwezo wa kutengeneza nafasi na pia kuwatoka mabeki wa timu pinzani.

Lakini wakati Uganda wakiwa na udhaifu na uimara huo, Stars kwa upande wake ina maeneo ambayo yanaweza kuibeba na yale ambayo inapaswa kuyafanyia kazi ili ifanye vizuri katika mchezo wa leo.

Udhaifu mkubwa wa Stars upo katika safu yake ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikipoteza nafasi wanazotengeneza pia safu ya kiungo imekuwa haijatengeneza muunganiko mzuri wa kitimu.

Pamoja na hilo, Stars inajivunia zaidi safu ya ulinzi inayoundwa na kipa Aishi Manula na mabeki Kelvin Yondani, Gadiel Michael, Mwaita Gereza na Bakari Mwamnyeto ambayo imekuwa imara katika kuwadhibiti wapinzani na kama itakuwa katika ubora huo, basi itawaweka katika wakati mgumu Uganda.

Rekodi kwa mechi ambazo zimekuwa zikizikutanisha zinaonyesha kuwa Stars imekuwa ikipata wakati mgumu mbele ya Uganda, pindi zinapokutana katika mashindano hayo ya Chalenji.

Katika mechi tano za mwisho kuzikutanisha timu hizo mbili, Uganda wameibuka na ushindi mara nyingi kulinganisha na Kilimanjaro Stars ambapo wamefanya hivyo mara tatu wakati Tanzania Bara imeibuka na ushindi mara mbili.

Katika kuonyesha kuwa Stars imekuwa ikipata wakati mgumu mbele ya Uganda, hata mara hizo mbili ambazo imeibuka na ushindi, ulitokana na mikwaju ya penati baada ya timu hizo mbili kumaliza kwa matokeo ya sare katika muda wa kawaida wa mchezo.

Mwaka 2013, Stars iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 3-2 baada ya mechi kwisha kwa sare ya mabao 2-2 na katika mchezo wa nusu fainali ambao ulizikutanisha mwaka 2010, Stars ilipata ushindi wa mikwaju ya penati 5-4 baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana dakika za kawaida za mchezo.

Lakini mara zote tatu ambazo Uganda wamepata ushindi, matokeo hayo yalikuwa katika muda wa kawaida wa mchezo wakishinda mabao 3-0 katika nusu fainali ya mwaka 2012 na nusu fainali ya mwaka 2011 wakiibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Kwenye mashindano ya mwaka 2009, timu hizo zilikutana katika hatua ya makundi ambapo Uganda waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Pamoja na rekodi hiyo, Kocha wa Uganda, Jonathan McKinstry alisema timu yake haiwadharau Kili Stars.

“Siku zote mechi baina ya Uganda na Tanzania huwa ngumu na mara ya mwisho timu hizi kukutana, Uganda tulipoteza hivyo hata mchezo huu wa nusu fajnali sidhani kama utakuwa rahisi ukizingatia pia wachezaji wangu wamecheza mechi nne mfululizo bila kupata nafasi ya kutosha kujiweka sawa na umri wao wengi ni wadogo.

“Hata hivyo tumejiandaa vizuri kuona ni kwa namna gani tutaibuka na ushindi dhidi yao na tuweze kutinga hatua ya fainali,” alisema McKinstry

Kocha wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda alisema kuwa timu yake haina presha wala hofu.

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...