
WAKATI ikigomea kumuuza mshambuliaji Allan Okello kwenda Azam kwa dau la Dola 100,000 zaidi ya Sh 230 milioni, KCCA ya Uganda imefichua kuwa imemweka sokoni beki wake wa kushoto Mustafa Kizza ambaye Yanga na Azam zinamtolea udenda.
Klabu hiyo imedai kuwa ni rahisi kwa Azam na Yanga kumchukua Kizza kwa sasa na wao wapo tayari kumruhusu aondoke lakini ikiwa watapatiwa dau linaloridhisha.
Ofisa Habari wa KCCA, Moses Magero alisema kuwa Kizza ni miongoni mwa wachezaji ambao Azam imeonyesha nia ya kuwahitaji na ikiwa watafikia makubalino, ataruhusiwa kujiunge nao.
“Sisi tuko tayari kumwachia mchezaji yeyote ajiunge na timu nyingine ikiwa italeta ofa inayoeleweka lakini kinyume cha hapo hatuwezi kuwa tayari kufanya hivyo kwa faida ya klabu na mchezaji mwenyewe.
“Kwa sasa ni vigumu kumuachia Allan Okello lakini kwa Kizza, Azam wanaweza kumpata kwani amebakisha mkataba wa mwaka mmoja wa kuendelea kuitumikia klabu yetu hivyo hatupendi aje kuondoka bure.
“Lakini hata hivyo kwa kiasi cha Dola 35,000 (Sh 80 milioni) ambacho Azam walikitenga kwa ajili ya kumchukua, hatuko tayari kumruhusu aondoke. Kama wao au timu nyingine yoyote ikiwa tayari kutoa fungu kubwa zaidi ya kiasi hicho cha fedha hatuwezi kumzuia Kizza,” alisema Magero akisisitiza anayemhitaji aifuate timu hiyo mezani.
No comments:
Post a Comment