MWITIKIO wa kiasili aliopata mshambuliaji wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang wakati wa mchezo wa ligi dhidi ya Brighton wiki iliyopita ulizua mjadala kwa mashabiki mitandaoni kuhoji kitendo hicho.
Zikiwa zimebaki dakika 10 mchezo kumalizika mshambuliaji huyo ambaye ni nahodha wa klabu hiyo alitoka nje ya uwanja na kwenda katika vyoo vilivyopo katika vyumba vya kubadilishia nguo.
Alitumia muda wa kama dakika tatu hivi kwenda katika mwito mfupi yaani kwa lugha rahisi kwenda kujisaidia haja ndogo huku timu yake ikiwa inaongoza goli 2-1.
Kocha wa muda wa Arsenal, Fredie Jumberg alionekana kutofurahishwa na tukio hilo ambalo ni nadra kuonekana katika viwanja vya mpira wa miguu.
Alipoulizwa Aubameyang alisema alikuwa katika shinikizo kubwa la kwenda haja kiasi cha kushindwa kustahimili hali hiyo.
Baadhi walikosoa hatua yake hiyo katika mtandao wa klabu hiyo wakidai hakikuwa kitendo sahihi kwani timu ilikuwa katika hatari ya kufungwa kwa kuwa na wachezaji pungufu.
Wapo waliomtetea wakisema kuwa hakuna mwanadamu anayependa kupata hali ile na ni vigumu kuizuia miito ya kiasili ikiwamo mwito mfupi na haja kubwa au ndogo.
Walieleza zaidi kuwa vitu hivi vinaweza kumtokea mtu yeyote katika muda wowote kwani ni kitendo ambacho mwili huamrisha kutokea na unaweza kukizuia kwa hiari yako lakini baadaye kibofu kikijaa kupitiliza mwili huamrisha haja hiyo kutoka pasipo hiari yako.
Lakini zaidi wengi wa wadau wa soka wamejiuliza je, hali ile ni kawaida au imetokana na ugonjwa unaosababisha kupata haja ya ghafla iliyomfanya kushindwa kustahimili.
Leo nitawapa ufahamu na namna mkojo unavyotengenezwa na mpaka unavyoweza kutolewa nje ya mwili na pia tutaona mambo yanayoweza kusababisha kupata haja ndogo ya ghafla.
Haja ndogo inavyotengenezwa
Kwa kawaida figo ndizo zinazohusika katika kulinda mazingira ya ndani ya mwili kwa kuondoa au kulinda kupotea kwa vitu mbalimbali vilivyopo katika damu.
Wakati wa uchujaji wa damu unaofika kwenye figo ndipo baadaye mkojo huzalishwa kama taka mwili ikiwa imesheheni vitu visivyohitajika mwilini.
Mfumo wa mkojo huwa na figo, mirija ya kuleta mkojo kutoka katika figo kuja katika kibofu ijulikanayo kama ureters na mrija wa kutolea mkojo nje ya mwili ujulikanao kama urethra.
Kitabibu mtiririko mzima wa kupata mkojo na kutoka nje ya mwili hujulikana kama micturition au voiding au urination.
Mkojo huwa na maji, chumvichumvi na takasumu za urea na taka nyingine za mwilini ikiwamo sumu zilizoingia mwilini.
Mkojo ni moja ya zao la taka mwili za mwili baada ya mfumo wa mkojo kuchuja damu inayopita katika figo iliyosheheni mirija midogomidogo na chujio.
Zipo hatua kuu tatu zinazohusika mpaka kupata mkojo. Hatua ya kwanza ni kuchujwa na kuondolewa vitu visivyohitajika. Hhatua ya pili ni mkojo kuchambuliwa na vitu muhimu kurudishwa tena mwili na hatua ya tatu ni chumvi au maji yaliyomo katika mkojo kuchukuliwa au kutolewa na vinavyobaki hutemwa katika kibofu kama zao la mwisho.
Katika kibofu, mkojo hurundikwa na pale unapojaa kupitia mishipa ya fahamu taarifa hufika katika ubongo na kupata tafsiri na baadaye amri hutolewa ili vibanio vya nje kibofu kufungua mkojo utoke.
Katika hatua hii inaweza kwa hiari kwa mtu binafsi kudhibiti mkojo lakini pale unapoubana mkojo hufikia mahali ni ngumu kuubana hatimaye pasipo hiari yako huamrisha mkojo kutoka.
Uhusiano kati ya mazoezi na haja ndogo
Kwa tathimini ya tukio la Aubameyang inaonyesha pengine alikuwa amekunywa maji mengi muda mfupi kabla ya kuingia uwanjani na tayari mwili ulikuwa na kiwango kikubwa cha kujitosheleza.
Na kipindi hiki hali ya hewa ya Ulaya ni ya baridi hali inayosababisha wachezaji kutopoteza maji mengi kwa njia ya jasho na badala yake wanapoteza maji na chumvichumvi wakati wa kupumua na kwa njia ya mkojo.
Kwa kufanya ulinganifu bado hakuna uhusiano wa mchezaji kupata haja ndogo ya ghafla na kufanya mazoezi au kucheza.
Inaonyesha kwa tukio lile upo uhusiano wa kupata haja ndogo na hali iliyopo sasa ambayo ni hali ya baridi na vilevile mchezaji mwenyewe upo uwezekano alikunywa maji mengi.
Nimetazama mechi za ligi iliyochezwa mwishoni mwa wiki pamoja na zile za mechi za Kombe la Carabao, Mabingwa wa Dunia na pamoja na mechi maarufu ya Ligi ya Hispania ya El Clasico.
Sikuweza kuona tukio lolote la kupata haja ndogo kwa wanasoka na kwenda kujisaidia kabla mechi kuisha au kabla ya mapumziko.
Hivyo, hapa tunapata picha kuwa hali ile inatokea kwa nadra sana na pengine kumtokea Aubameyang haikua jambo la kila mara.
Kwa kawaida wanasoka wengi hujisaidia kabla ya kuanza kwa mchezo, wakati wa mapumziko na baada ya mchezo kumalizika.
Aubameyang alieleza kuwa alishindwa kuvumilia shinikizo la haja ndogo kali aliyomkaba, hivyo alilazimika kwa hiari kutoka na kwenda kujisaidia kabla ya mchezo kwisha.
Nini kitatokea unapouzuia mkojo?
Kwa upande wa sayansi ya tiba ya mfumo wa mkojo inaonyesha endapo mkojo unapojaa kupita kiasi hufika hatua badala ya mtu kwa kukojoa kwa hiari yake mwili wenyewe kupitia mfumo wa fahamu huamrisha mkojo kutolewa pasipo hiyari ya mtu.
Mwili hufanya hivi kwa lengo la kuzuia madhara kwani mkojo unapojaa sana katika kibofu huleta maumivu makali sana yasiyovumilika na pia mkojo ni taka sumu ambayo mwili hauhitaji.
Endapo Aubameyang angeliendelea kujizuia pengine angeliweza kujikojolea jambo ambalo lingekua gumzo zaidi na ingelimletea fedheha.
Kukabwa na haja ndogo ya ghafla mchezoni si tatizo la kiafya bali ni mwili wa mtu mwenyewe kuwa na maji mengi mwilini na mwili kutumia njia ya mkojo kupunguza maji yaliyozidi.
Aubameyang hana tatizo lolote la kiafya hali iliyomtokea ni ya kawaida.
No comments:
Post a Comment