
WATANZANIA wanapenda sana soka. Soka na michezo mingine zimekuwa zikileta na kuhamasisha amani, undugu na kuwaunganisha watu wote bila kujali rangi, jinsia wala itikadi zingine.
Hata hivyo, soka la Tanzania limekuwa na changamoto nyingi na za muda mrefu ambazo kwa namna moja ama nyingine zimekuwa zikilitia doa.
Miongoni mwa changamoto ambazo zimekuwa sugu kwenye soka letu ni upangaji wa ratiba hasa za mechi za Ligi Kuu Bara.
Licha ya ratiba kutolewa mapema kabisa kabla ya kuanza kwa ligi, lakini siku chache ama baada ya michezo miwili ni lazima ipanguliwe.
Tunatambua zipo sababu mbalimbali zinazosababisha ratiba kupanguliwa, lakini nyingi hazina mashiko kwa kuwa hazipo kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) ama lile la Afrika (Caf). Katika mataifa yaliyoendelea ni nadra sana kukuta ratiba inapanguliwa kwa sababu ambazo hazina mashiko kama ilivyo huku kwetu, labda itokee sababu ambazo haziwezi kuzuilika hasa majanga ya kiasili.
Lakini, kwa Tanzania mambo ni tofauti kabisa kwani, klabu inaweza kuandika barua kuomba mchezo wake usogezwe mbele na Bodi ya Ligi ikaridhia.
Klabu inaweza kuandika barua ikidai wachezaji wake wawili ama watatu wameitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) na ikakubaliwa ama ikaomba inakwenda kushiriki kwenye mechi za mwaliko.
Yaani ili mradi kila mmoja anapopanga lake basi lazima likubaliwe na hapo ndipo tunapokutana na majanga.
Katika kuthibitisha hili ikiwa ni kelele za muda mrefu sasa, jana Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kumsimamisha Ofisa wake, Joel Balisidya kutokana na kuhusika na uzembe uliopelekea mabadiliko ya ghafla ya mchezo wa Ligi Kuu Bara baina ya Azam FC na JKT Tanzania, Jumapili, Disemba Mosi.
Mechi hiyo awali ilipaswa kuchezwa saa 1.00 usiku, lakini ghafla kukawa na mabadiliko na ikachezwa saa 10.00 jioni jambo lililolalamikiwa na Azam FC hasa baada ya kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Mwenyekiti wa TPLB, Steven Mnguto alisema kuwa bodi inawajibika kwa uzembe uliojitokeza na imeamua kuchukua hatua kwa aliyesababisha.
Imeelezwa kwa bahati mbaya, taarifa kwenda kwa Azam TV ilikwenda kitofauti kwa kuonyesha saa 10.oo jioni badala ya saa 1.00 usiku. Kwa mujibu wa Mnguto haikuwa taarifa ya mdomo bali ya maandishi ambayo ilitoka bodi. Japo hili linahitaji utetezi wa ziada kwa kuwa, ni lazima nakala ya barua hiyo iliyokwenda Azam ilipaswa kuonwa na maofisa wengine wa Bodi ambao, walipaswa kuhoji kabla ya utekelezaji wake.
Kama nakala ya barua hiyo haikuambatanishwa kwa maofisa wengine wa Bodi kwa ajili ya kuweka rekodi ama kutoa ushauri basi kunaashiria kuna tatizo la kiutendaji ndani ya chombo hicho muhimu.
Hata hivyo, Mwanaspoti linaikumbusha TFF na Bodi ya Ligi, wanapaswa kuchukua hatua pindi wanapoona makosa ya kizembe kama hayo badala ya kusubiri malalamiko.
Azam na wachezaji wao wamelalamikia mabadiliko hayo ya ghafla na kushusha mzigo wa lawama, matokeo hayo ya sare ya 2-2 dhidi ya Polisi Tanzania chanzo ni kubadili muda kutoka saa 1.00 usiku kwenda saa 10.00 jioni huku wachezaji wakifanya mazoezi kulingana na ratiba ya mechi.
No comments:
Post a Comment