
LONDON, ENGLAND . STRAIKA, Pierre-Emerick Aubameyang anajipanga kuachana na Arsenal baada ya kujitoa kwenye mazungumzo ya kuhusu mkataba mpya kwenye kikosi hicho cha Emirates.
Staa huyo wa kimataifa wa Gabon, Aubameyang amefunga mabao 53 katika mechi 83 alizoitumikia Arsenal tangu alipojiunga Januari 2018 akitokea Borussia Dortmund, lakini anataka kuondoka kwa sababu anataka timu inayoshindania mataji.
Na sasa mipango yake ni kuachana na wababe hao wa Emirates kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi mwishoni mwa msimu huu.
Aubameyang alishinda Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England msimu uliopita na msimu huu ameonyesha kuwa moto akiwa amefunga mabao 12 katika mechi 17 alizoitumikia timu hiyo ya London.
Mkataba wake umebakiza miezi 18 tu kufika tamati, lakini hali yake ya mambo huko kwenye kikosi hicho ipo njiapanda akitaka zake kuondoka kutokana na mambo kutoeleweka. Aubameyang alinaswa kwa Pauni 56 milioni, lakini anaona timu kila siku inazidi kurudi nyuma tu na yeye mipango yake ni kubeba mataji.
Kwenye maisha yake ya soka, Aubameyang, amebeba Kombe la Ligi Ufaransa na Kombe la Ujerumani, hivyo anataka kunyakua taji kubwa zaidi kabla ya kuachana na mchezo huo, ambapo ikifika Juni mwakani atafikisha umri wa miaka 31.
Aubameyang anaripotiwa kutaka kuondoka wakati zimepita wiki chache tu tangu alipoteuliwa kuwa nahodha kwenye kikosi hicho. Arsenal imeshinda mechi nne tu kati ya 15 ilizocheza kwenye Ligi Kuu England na kesho Jumatatu watakuwa na shughuli ya kuwakabili West Ham United ugenini.
No comments:
Post a Comment