London, England. Kocha Carlo Ancelotti amesema atavunja rekodi ya Jurgen Klopp kwa kuifunga Liverpool katika mchezo wa Ligi Kuu England.
Ancelotti ametoa kauli hiyo baada ya kutangazwa kocha mpya Everton akijaza nafasi ya Marco Silva aliyefukuzwa.
Mtaliano huyo akiwa Napoli aliiongoza kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Liverpool katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Septemba, mwaka huu.
Ancelotti alisema anataka kuendeleza ubabe kwa Klopp katika Ligi Kuu England kwa kuwa tayari anazijua mbinu za Mjerumani huyo.
Ancelotti ana rekodi ya kushinda mechi saba kati ya 12 dhidi ya Liverpool katika historia yake ya ukocha. Everton itaifuata Liverpool Uwanja wa Anfield kuikabili katika mchezo wa Kombe la FA Januari 5.
“Wadau wa Everton wajua rekodi yangu dhidi ya Liverpool. Najua mashabiki wake walivyokuwa na kiu ya kutaka ushindi, hatuna sababu tunawasubiri Januari 5,”alisema Ancelotti.
Alisema itakuwa mechi ngumu, lakini anaona fahari kuwakabili wapinzani wao katika mchezo huo wa Kombe la FA. Mara ya mwisho Everton kuifunga Liverpool Anfield ilikuwa mwaka 1999.
Ancelotti aliifunga mara mbili Liverpool akiwa Napoli, mara mbili (Real Madrid), mara mbili (Chelsea) na mara moja akiwa AC Milan mwaka 2007 katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
No comments:
Post a Comment