
LONDON, ENGLAND . KAMA unadhani kwamba matatizo ya Arsenal hali haitakuwa mbaya zaidi, basi unakosea maana hivi unavyosoma hapa straika wao na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang amegoma kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea timu hiyo.
Arsenal wamekuwa na wakati mzuri kutokana na mabao ya mshambuliaji huyo, lakini suala la kwanza kumpoteza ni jambo linalozua presha kubwa kwenye timu na kwa mashabiki wao kwa ujumla. Straika, Aubameyang anataka kuachana na Arsenal kwa sababu mpango wake ni kwenda kuchezea timu itakayompa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na kama siyo hivyo, basi timu itakayompa pesa ndefu katika kipindi hicho ambacho umri nao unazidi kumtupa mkono.
Wakati ukijiuliza Aubameyang atatimkia wapi wakati wake wa kuitumikia Arsenal utakapofika mwisho baada ya kugomea kusaini mkataba mpya, huku ndiko anakoweza kuibukia, ikiwamo Paris Saint-Germain, Juventus na Bayern Munich.
Man United
Kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi kulikuwa na uvumi unaomhusisha straika huyo kwenda Manchester United. Kilichokuwa kikielezwa kwamba Aubameyang alikuwa anakwenda kufuata nyayo za Robin van Persie kwa kuachana na Arsenal na kwenda kujiunga na Man United.
Dili hilo lilishindwa kukamilika kwa wakati huo, lakini kwa sasa kocha Ole Gunnar Solskjaer anahitaji mtu wa kwenda kumfungia mabao kwenye kikosi chake hivyo, hivyo anaweza kuibukia kwa straika huyo wa Gabon baada ya kuwapo kwa taarifa za kugomea kusaini mkataba mpya huko Emirates. Aubameyang mwenyewe kuna uwezekano mkubwa wa kushawishika kwenda Old Trafford.
Real Madrid
Taarifa za kutoka huko Hispania zimekuwa zikizungumzia kwa karibu kuhusu ishu ya maisha ya Aubameyang huko kwenye kikosi cha Arsenal. Mara kadhaa, Real Madrid wamekuwa wakiripotiwa kuhitaji huduma yake kwenda kusaidia na Karim Benzema kwenda kufanya kazi moja ya kufunga mabao huko Santiago Bernabeu. Kitu kinachowapa moyo Real Madrid ni kuhusu ripoti za kwamba Arsenal wamemruhusu Aubameyang kuondoka kama kutakuwa na ofa nzuri huko rais wa wababe hao wa Bernabeu, Florentino Perez, akijiandaa kutumia Euro 80 milioni katika kunasa huduma ya nahodha huyo wa Arsenal, ambaye imedaiwa amekuwa akikumbali kupita maelezo. Kitendo cha kuelezwa kwamba Aubameyang anapatikana basi Real Madrid wapo tayari kulipa kiasi chochote cha pesa.
Anapokuwa kwenye ubora wake, Luis Suarez ni straika asiyekamatika uwanjani. Lakini, kwa bahati mbaya umri sasa umeshaanza kumtupa mkono supastaa huyo wa kimataifa wa Uruguay. Kutokana na hilo, Barcelona wamekuwa wakihaha kutafuta mshambuliaji anayefaa kwenda kuziba pengo lake, wametajwa wengi na mmoja wao ni Aubameyang.
Na hali ya mambo ilivyo, Barcelona hawapo tayari kusubiri hadi mwisho wa msimu baada ya kuona kwamba Antoine Griezmann ameshindwa kufanya kazi wanayotaka na huenda wakaingia sokoni dirisha la Januari kwenda kunasa huduma ya mshambuliaji huyo. Arsenal wenyewe wanafahamu hakuna namna zaidi ya kumpiga tu bei fowadi wao huyo kama amegoma kusaini dili jipya la kubaki Emirates. Mkataba wake unaisha 2021.
Inter Milan
Kwa mujibu wa Tuttomercatoweb, Aubameyang amekuwa akiwindwa na miamba ya soka ya Italia, Inter Milan ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa karibu maendeleo yake Arsenal. Barcelona wanamtaka straika Lautaro Martinez, hivyo Inter wao wanaamini watakapompoteza mshambuliaji wao huyo, basi hakutakuwa na ujanja zaidi ya kuwa na huduma ya Aubameyang. Kwenye mchakato huo ni suala la Barca kuamua kama watakwenda moja kwa moja kwa Aubameyang, basi Inter Milan watabaki na staa wao Lautaro Martinez, lakini kama watavamia kwenye kikosi chao na kumnasa Muargentina huyo, kocha Antonio Conte hatakuwa na chaguo jingine zaidi ya kutimkia zake Emirates kumng’oa fowadi huyo moto kabisa England.
Shanghai SIPG
Kauli ya Aubameyang kutaka kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya haina maana kwamba hatakuwa tayari kwenda timu nyingine kama itaweka mezani ofa ya mkwanja mrefu.
Ukweli ni kwamba kauli ya Aubameyang kusema anataka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya ameitoa kiujanja tu kukwepa kusema kwamba hataki tena kuichezea Arsenal, kwa sababu ni wazi kwa msimu ujao kuna nafasi ndogo ya timu hiyo ya Emirates kufuzu michuano hiyo ya Ulaya.
Auba pia anahitaji dili tamu mezani jambo hilo ndipo inapokuja klabu ya China ya Shanghai SIPG, ambapo waliwahi kuripotiwa kumpa straika huyo ofa ya kumlipa mshahara wa Pauni 300,000 kwa wiki akakipige kwenye kikosi chao. Kuna timu nyingine kibao za kutoka Mashariki ya Mbali ambazo zimekuwa zikihitaji saini ya mshambuliaji huyo ikiwamo Guangzhou Evergrande na Tianjin Quanjian ambazo ziko tayari kutoa mkwanja mrefu.
Atletico Madrid
Kumekuwa hakuna taarifa nyingi sana za kuhusu Aubameyang kwenda Atletico Madrid, lakini kwenye soka
chochote kinaweza kutokea kutokana na miamba hiyo ya La Liga kuhitaji huduma za mastaa ambao wana uwezo mkubwa katika kufunga mabao. Atletico imekuwa timu moto kwa kuwa washambuliaji wa kati wenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao na sasa wanaweza kugeukia kwa Aubameyang kwenye kusaka huduma yake.
Straika wao wa sasa Diego Costa anapiga hesabu za kwenda kujiunga na Flamengo, jambo hilo litawafanya Atletico kutokuwa na namna nyingine zaidi ya kuhamia kwa Aubameyang katika kusaka mtu wa kwenda kuziba pengo lake huku akienda kusaidiana na wakali wengine kama Joao Felix kwenye kikosi hicho cha Wanda Metropolitano.
No comments:
Post a Comment