
ZURICH, USWISI . SHIRIKISHO la soka la Ulaya, UEFA limetangaza kikosi chake cha kwanza cha muda wote cha Ligi ya Mabingwa Ulaya na kitu cha kushangaza ni kwamba kuna Mwingereza mmoja tu.
Makocha wa timu za Ulaya wametengeneza kikosi hicho cha kwanza cha wachezaji waliokuwa wamechaguliwa na mashabiki kwenye timu za mwaka kwa kuanzia mwaka 2001.
Kikosi hicho kinaundwa na supastaa, Cristiano Ronaldo, mshindi mara tano wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushinda mara nne akiwa na Real Madrid na mara moja alipokuwa na Manchester United .
Wachezaji wenzake wa zamani huko Real Madrid, beki wa kati Sergio Ramos na kipa Iker Casillas wametajwa kwenye timu, lakini ikiwa na mastaa kibao wa kutoka Barcelona, kuanzia Lionel Messi, Andreas Iniesta na Xavi waliobeba mara nne taji hilo kila mmoja sambamba na Gerard Pique, ambaye alibeba mara moja akiwa na Man United na mara tatu akiwa na Barca na kuungana pia na Carles Puyol.
Mwingereza pekee aliyeingia kwenye kikosi hicho ni gwiji wa Liverpool, Steven Gerrard, ambaye aliisaidia timu hiyo kutoka nyuma kwa mabao 3-0 kwenye fainali ya mwaka 2005 na kisha kushinda kwa penalti dhidi ya AC Milan huko Istanbul. Staa mwingine wa zamani wa kutoka kwenye Ligi Kuu England, aliyejumuishwa kwenye kikosi hicho ni Thierry Henry, ambaye ataunda ile safu ya washambuliaji ya mastaa watupu itakayojumuishwa na Messi na Ronaldo.
Ronaldo alichaguliwa kwenye timu za mwaka za Uefa mara 13 tofauti, wakati Messi amechaguliwa mara 10 na Henry mara tano. Casillas amechaguliwa mara sita, Ramos mara nane. Pique mara tano, Puyol (sita) na beki wa kushoto wa zamni wa Bayern Munich, Philipp Lahm mara tano, wakati Iniesta mara sita na Xavi mara tano.
Kikosi chenyewe cha muda wote cha Uefa hiki hapa: Casillas; Ramos, Pique, Puyol, Lahm, Gerrard, Xavi, Iniesta, Ronaldo, Messi, Henry.
No comments:
Post a Comment