
LONDON, ENGLAND . STRAIKA kinda wa Chelsea, Tammy Abraham amekuwa hatari kwa kutikisa nyavu huko kwenye Ligi Kuu England na michuano mingine, lakini mwenyewe amefichua siri ya mafanikio yake ya kuwa mtikisa nyavu hatari.
Fowadi huyo aliyekuwa amefunga mabao 12 ya michuano yote kabla ya mchezo wa jana Jumatano usiku kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ugenini kwa Valencia amedai kwamba amekuwa akitazama video za YouTube za wakali watatu, Harry Kane, Sergio Aguero na Roberto Firmino na kisha kuiga kile wanachofanya uwanjani na hilo ndilo linalomfanya kuwa bora.
Ahraham ameonyesha kuwa ni moto kwenye kufunga ambapo kwenye Ligi Kuu England ametikisa nyavu mara 10 na kuwa kwenye orodha ya virana wa mabao wanaofukuzia Kiatu cha Dhahabu cha ligi hiyo msimu huu.
Mwenyewe alisema hivi: “Katika muda wangu wa mapumziko, nimekuwa nikiingia kwenye Youtube na kuangalia video za washambuliaji hatari duniani wanavyocheza kwenye mechi kubwa, naiba mbinu zao na kuongeza za kwangu.
“Naangalia mara nyingi sana. Harry Kane, Aguero, Firmino, hawa ndio washambuliaji ninaowatazama mara kwa mara kwenye Ligi Kuu England, lakini nimekuwa nikimtazama pia Lewandowski na washambuliaji wengine moto kwa kufunga."
Straika Abraham amekuwa moto huko kwenye kikosi cha Chelsea baada ya kocha Frank Lampard kumpa nafasi ya kuonyesha ubora wake na kitendo cha kumwaamini kimekuwa na faida kubwa kwake na kuwa mfungaji mahiri wa kikosi hicho. Kinara wa mabao kwenye ligi hiyo msimu huu, Jamie Vardy ndiye pekee aliyemzidi Abraham, akiwa amefunga mabao mawili zaidi ya yale yaliyofungwa na kinda huyo matata wa Stamford Bridge.
No comments:
Post a Comment