
Dar es Salaam.Kama we ni shabiki wa nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Diamond Platunumz, bila shaka unajua ngoma yake ya 'Baba Lao' inavyosumbua kwa sasa hewani.
Ni ngoma moja matata ambayo ilitoka kipindi akijiandaa kupiga shoo yake ya Wasafi Festival ya jijini Dar es Salaam.
Kama Chibu Dangote anajinasibu ni baba lao, basi unaambiwa kwenye Ligi Kuu Bara kuna Baba Lao lililofunika vigogo wote mpaka sasa! Hao Simba, Yanga, Azam na Mtibwa Sugar wote wamekaa kwa rekodis za Prisons.
Maafande wa Tanzania Prisons ya jijini Mbeya ndio Baba Lao katika ligi ya msimu huu iliyoingia raundi ya 12, ikiwa ni timu pekee ambayo haijaonja kipigo katika mechi zake.
Mabingwa wa Kihistoria, Yanga waliotwaa taji la Ligi Kuu mara 27 wamechapika kwa Wazee wa Kupapasa, Ruvu Shooting. Watetezi wa ligi na wanaoshika nafasi ya pili kwa kutwaa mara nyingi taji la michuano hiyo, Simba wenyewe nao wameshapigika kwa Mwadui ya Shinyanga.
Matajiri wa Chamazi, Azam FC wao ndio wameumia vibaya miongoni mwa vigogo, kwani wamenyooshwa mara mbili dhidi ya Ruvu na Simba, ilihali Mtibwa Sugar waliwahi kunyakua taji mara mbili, wamefungwa mara nne, kuonyesha upepo umewakataa mapema.
Lakini vidume vya Prisons wanaonolewa na Kocha Mohammed 'Adolph' Rishard, wao wamekomaa kinoma, licha ya kwamba ni moja ya timu ambayo imepoteza pointi nyingi kwa kutoka sare nyingine mpaka sasa katika ligi hiyo, lakini ndio pekee ambao hawajafungwa mpaka sasa.
Mara ya mwisho kwa Prisons kuonja kipigo ni mechi yao ya pili kabla msimu uliopita haujafungwa walipoenda kulala ugenini walipolambwa bao 1-0 na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga kwa bao la dakika 70 la Raizin Hafidh.
Mechi hiyo ilipigwa Mei 23 mwaka huu na baada ya hapo maafande hao wameamua kukomaa kwa kutofungwa tena, na leo Jumapili wametimiza siku 185 wakicheza mechi 12 za Ligi bila kipigo.
Wala usibishe sana, we chungulia hapo chini uone rekodi za mechi hizo na kile walichokivuna ndani ya siku hizo 185.
Mei 28, 2019
Prisons 3-1 Lipuli
Ago 24, 2019
Mbeya City 0-0 Prisons
Sep 15, 2019
Prisons 2-1 Ruvu Shooting
Sept 25, 2019
Mtibwa 1-3 Prisons
Sept 29, 2019
Lipuli 2-2 Prisons
Okt 19, 2019
Prisons 1-1 Kagera Sugar
Okt 23, 2019
Prisons 0-0 Biashara Utd
Okt 28, 2019
Alliance 1-1 Prisons
Okt 31, 2019
Mbao FC 1-1 Prisons
Nov 03, 2019
JKT Tanzania 0-1 Prisons
Nov 07, 2019
Simba 0-0 Prisons
Nov 22, 2019
Prisons 1-1 Mwadui
Ilichovuna katika mechi zake bila kupoteza
P W D L F A PTS
Prisons 12 4 8 0 15 9 20
No comments:
Post a Comment