
LONDON, ENGLAND . MAURICIO Pochettino amewaachia ujumbe wenye hisia kali wachezaji wa Tottenham Hotspur alipouandika kwenye ubao wa kujifunzia uliopo kwenye vyumba vya kubadilishia baada ya kushtukizwa kwa tukio la kufutwa kazi.
Kibarua cha ukocha wa Pochettino huko Spurs kilifika mwisho Jumanne usiku wakati alipoondolewa na asubuhi tu ya siku inayofuata, Jose Mourinho alitangazwa kuchukua nafasi yake.
Aliyekuwa msaidizi wake huko Spurs, Jesus Perez, alituma picha inayomwonyesha Pochettino akiandika ujumbe huo wenye hisia kwa ajili ya wachezaji kwa sababu hakupata nafasi ya kuagana nao. Pochettino na benchi lake lote la ufundi limefutwa kazi.
Ujumbe huo wa Poch ulisomeka hivi: "Asanteni sana kwenu nyote!"
"Hatuwezi kuagana...siku zote mtabaki kwenye mioyo yetu."
Kisha akaweka saini yake, jambo lililowagusa mastaa wengi wa Spurs, akiwamo straika wao, Harry Kane, ambaye alitumia ukurasa wake wa Twitter kuandika: "Kocha. Siku zote nitakushukuru kwa kunisaidia kufikia ndoto zangu. Tumekuwa na nyakati nzuri ndani ya miaka mitano na nusu na sitasahau. Ulikuwa kocha wangu, rafiki yangu na hakika nashukuru kwa hilo.
Kipa, Paulo Gazzaniga aliongeza: "Asante kwa kuniamimi na kunifanya nijifunze mengi kutoka kwako ndani na nje ya uwanja. Nawatakia kila la heri, Mauricio, Toni, Miguel na Jesus."
Lakini, kocha aliyekuja kuchukua mikoba yake, Mourinho naye amekuwa na kitu cha kusema kuhusu Pochettino, akisema: “Kwa masikitiko makubwa, lakini ni lazima nimzungumzie Mauricio. Nampongeza kwa kazi kubwa aliyofanya. Klabu hii siku zote itakuwa nyumbani kwake, uwanja wa mazoezi utakuwa wake na siku zote milango itakuwa wazi kwake.
"Anaweza kuja muda wowote anaotaka. Akiwakumbuka wachezaji, akiwakumbuka watu aliokuwa anafanya nao kazi, milango ipo wazi. Naamini atapata furaha tena, atapata timu kubwa na atakuwa na kitu kizuri hapo baadaye."
No comments:
Post a Comment