WAKATI bondia Hassan Mwakinyo akitamba kumkalisha mapema mpinzani wake Arnel Tinampay leo, bondia mwingine wa Tanzania Mfaume Mfaume ameonekana kuliteka pambano hilo.
Dalili za Mfaume kuliteka pambano la Mwakinyo zilianza kuonekana jana wakati mabondia hao wakipima uzito kwa ajili ya mapambano ya leo kwenye ofisi za Azam Tv zilizopo Tabata, Dar es Salaam.
Mfaume mwenye maskani yake Mabibo jijini humo atapanda ulingoni katika pambano la utangulizi dhidi ya mpinzani wake Keis Ally wa Manzese katika pambano la raundi nane la uzito wa Super Welter.
Licha ya pambano kubwa linalotajwa kuwa ni la Mwakinyo na Mfilipino, lakini hali ilikuwa tofauti kwenye ofisi za Azam Tv wakati mabondia wote walipokwenda kupima uzito baada ya mashabiki wengi kumsindikiza Mfaume.
Bondia huyo alitangulia kufika kwenye ofisi za Azam TV akiwa na farasi akifuatiwa na gari aina ya Fuso lililokuwa limebeba mashabiki mchanganyiko waliokuwa wakipiga ngoma wakifutiwa na magari mengine na pikipiki, lakini hata hivyo mashabiki wa bondia huyo wajikuta wakizuiwa na walinzi wa getini katika ofisi hizo kwa kuwaambia hawawezi kuingia.
Mashabiki hao walianza kulumbana na walinzi hao wakilazimisha kutaka kuingia ndani, lakini wakagomewa na nusura wavunje geti la Azam TV kabla ya kudhibitiwa na kuwa wapole.
Baada ya shughuli ya kupima uzito kumalizika, Mfaume alitoka akiwa na farasi wake na kupokewa na mashabiki wake lukuki nje ya geti na hivyo safari ya kuelekea Mabibo yalipo makazi ya bondia huyo ilianza, hivyo kusababisha foleni kubwa barabarani kwani magari na pikipiki zilitanda barabara yote huku zikienda taratibu kama wanasindikiza harusi.
Mfaume ni kipenzi cha mashabiki wengi huku akijizolea umaarufu baada ya kumchapa Mohammed Matumla mpaka kusababisha kulazwa hospitali baada ya kupasuka sehemu ya fuvu la kichwa katika pambano lililofanyika Februari 9, 2017.
Nusura Mfilipino
amgomee Mwakinyo
Jana mabondia hao walipima uzito kwenye ofisi hizo na Tinampay ndiye aliyeanza kupima na kubainika kuwa na kilo 69.7, kisha akafuatia Mwakinyo ambaye baada ya kupima alikuwa na kilo 70.6.
Baada ya Mwakinyo kushuka kwenye mzani, Mfilipino aliambiwa kupitia mkalimani wake na kuonekana kuingiwa na wasiwasi, hivyo kutaka apime tena ndipo wasimamizi wa suala hilo walioongozwa na Raisi wa Kamisheni za Ngumi Tanzania, Joe Anea walimruhusu na mabondia wote kupima upya na majibu kuwa vilevile
Mfilipino huyo alipoulizwa anakubali kupambana na Mwakinyo licha ya kwamba alizidiwa uzito kwa kilo moja, alinyamaza kwa sekunde kadhaa na kushauriana vitu kadhaa na wenzake kabla ya baadaye kukubali.
Mwakinyo awapa makavu Mondi, Kiba
Bondia Mwakinyo ni kama anaumizwa na jinsi wasanii wakubwa wa muziki hapa nchini wanashindwa kutoa sapoti katika mchezo huo tofauti na wenzao kutoka nje ya nchi.
“Kuna sapoti ndogo sana hapa nchini kwetu kwani ukiangalia sisi ni mabondia ambao tunamsikiliza Diamond, Ali Kiba, Ommy Dimpoz na wengine wengi na mara kwa mara tunacheza nyimbo zao pia, lakini hatuwaoni katika matukio kama haya,” alisema bodia huyo.
“ Ukizingatia sisi tunafanya vitu kwa niaba ya Watanzania na tunasapoti kazi zao na wao ilipaswa wasapoti kazi zetu kwa sababu tuko pamoja kulijenga taifa.”
No comments:
Post a Comment