
LONDON, ENGLAND . ISHU ya kocha mkuu mpya wa kudumu huko Arsenal inazidi kunoga. Majina kibao yamekuwa yakitajwa tangu alipofutwa kazi Unai Emery na sasa Max Allegri anadaiwa kwamba ndiye anayeongoza kwenye kinyang'anyiro hicho cha kuchukua mikoba ya kuinoa The Gunners.
Emery hakuwa na namna nyingine zaidi ya kufutwa tu kazi kufuatia timu kuchapwa 2-1 nyumbani Emirates kwenye mchezo wa Europa League dhidi ya Eintracht Frankfurt huku timu hiyo ikiwa imecheza mechi saba bila ya kupata ushindi.
Kikosi hicho kwa sasa kipo chini ya Fredrik Ljungberg kwa muda na huenda akabaki kwenye timu hiyo mwishoni mwa msimu, lakini ni nani atakayekuja kuchukua mikoba ya jumla itakapofika Agosti 2020?
Kuhusu Ljungberg kupewa kazi ya kudumu anapewa nafasi ya tatu, huku Max Allegri akiwaongoza na kufuatia na Espirito Santo wa Wolves. Mauricio Pochettino, aliyefutwa kazi Tottenham, naye tupo kwenye orodha ya makocha wanaopewa nafasi za juu kuchukua mikoba hiyo sawa na Mikel Arteta.
Kocha wa Leicester City, Brendan Rodgers naye anapewa nafasi, lakini kwa Arsenal kunasa huduma yake watalazimika kulipa fidia ya Pauni 14 milioni kitu ambacho mabosi wa timu hiyo ya Emirates wanaweza kujifikiria sana kama waliona hasara kumfuta kazi mapema Emery kwa sababu tu watatakiwa kulipa Pauni 4 milioni. Carlo Ancelotti, Rafael Benitez na Patrick Vieira ni makocha wengine wanaohusishwa na kibarua hicho cha kudumu cha kuinoa Arsenal.
Kocha Emery ameshindwa kufanya maajabu wakati alipopewa majukumu ya kuvaa buti za Arsene Wenger baada ya kuachana na timu hiyo.
Rekodi za Emery kwenye mechi 51 alizosimamia timu kwenye Ligi Kuu England, hazina tofauti kabisa na mechi 51 za mwisho za Wenger kwenye timu hiyo.
Makocha hao wote walivuna pointi 88, lakini Wenger akishinda mechi 27 na Emery 25. Emery ametoka sare 13 na kupoteza mara 13, huku akifunga mabao 91, wakati Wenger alitoa sare saba na kuchapwa mara 17 huku timu yake ikifunga mabao 97. Lakini, mwisho wa yote, pointi zilikuwa sawa, 88 na kuonekana kama vile hakuna kilichobadilika, huku Arsenal ya Wenger ilipata ushindi kwenye mechi mbili zaidi ya Arsenal ya Emery.
Baada ya Emery kufutwa kazi, mashabiki kibao wa Arsenal walitumia kurasa zao za Twitter kueleza hisia zao, huku mmoja aliandika: "Nimeshuhudia Arsenal ikiwasajili Bendtner, Andre Santos, Gervinho, Chamakh, Senderos, Sanogo, Gazidis kama mkurugenzi mtendaji mkuu, lakini kitu cha hovyo zaidi ni Unai Emery. Aende tu."
No comments:
Post a Comment