
Dar es Salaam. Mabingwa Watetezi wa mashindano ya Afrika Mashariki na Kati kwa wanawake, timu ya taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Queens' imeanza vyema mashindano hayo mwaka huu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 9-0 dhidi ya Sudan Kusini kwenye Uwanja wa Chamazi jijini.
Huku ikionyesha kiwango bora katika mechi hiyo ikimiliki mpira, kutengeneza nafasi na kucheza kwa kasi kubwa ambayo iliwaweka Sudan Kusini katika wakati mgumu kwenye sehemu kubwa ya mchezo.
Kilimanjaro Queens ilionyesha mapema uchu wa mabao katika mchezo huo na ilithibitisha hilo kwa kwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa mabao matatu yaliyofungwa na Mwanahamisi Omary 'Gaucho' aliyepachika mawili na Donisia Daniel aliyepachika moja katika dakika ya 16, 36 na 42.
Kilimanjaro Queens walirudi kipindi cha pili wakionekana wamepania zaidi na waliangusha kalamu ya mabao kwa kufunga jumla ya mabao sita huku wakipoteza idadi kubwa ya nafasi za mabao.
Mabao ya Opa Clement na Stumai Abdallah waliofunga mawili kila mmoja na Gaucho na Julitha Tamuwai yalihitimisha ushindi huo mnono kwa Kilimanjaro Queens ambao umeifanya iongoze kundi A mbele ya Burundi ambayo katika mchezo wa awali iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Zanzibar.
Kocha wa Kilimanjaro Queens, Bakari Shime alisema kuwa vijana wake walistahili kupata matokeo hayo ya ushindi.
"Nadhani baada ya kupata mabao tisa vijana wangu walionyesha hali ya kuridhika na kushindwa kuongeza mengine zaidi.
Kwetu sisi matokeo sio kitu kikubwa zaidi ya namna gani timu inavyoonyesha muunganiko na inavyofanyia kazi mbinu tunazowapa," alisema Shine
No comments:
Post a Comment