Search This Blog

Friday, November 22, 2019

Daniel Maldini : Mtoto wa Paolo Maldini aliyeanza kutesa San Siro

MILAN, ITALIA . KIZAZI kingine cha Maldini kimeanza kutesa tena. Safari bado ni ndefu kwa kizazi hiki kuendelea kutesa Italia.

Daniel Maldini, mtoto wa staa wa zamani wa AC Milan na timu ya taifa ya Italia, Paolo Maldini ameanza kuzua gumzo kutokana na kiwango anachoonyesha katika timu ya vijana ya AC Milan huku akianza kugusagusa katika kikosi cha wakubwa. Ametokea wapi Daniel?

Azaliwa Milan, akulia Milan

Daniel alizaliwa Oktoba 11, 2001 katika jiji la Milan baba yake akiwa Paolo Maldini wakati mama yake akiwa Adriana Maldini ambaye ni mke wa Paolo mpaka sasa. Daniel ana umri wa miaka 17 na alianza kucheza soka la watoto katika klabu hiyo wakati baba yake akielekea kustaafu soka.

Baba yake, Paolo ni mmoja kati ya wachezaji bora wa muda wote katika soka la Italia akiwa ameichezea AC Milan mechi 902 na kutwaa mataji 26. Kwa sasa ni Mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo ambayo ni klabu pekee aliyoichezea katika maisha ya soka.

Daniel anakuja Milan akiwa mwendelezo wa kizazi cha kwanza cha Maldini klabuni hapo ambapo babu yake, Cesare Maldini, baba wa Paolo Maldini alikuwa staa pia klabuni hapo kati ya mwaka 1954 hadi 1966. Cesare aliichezea AC Milan mechi 412 na pia kuifundisha AC Milan katika vipindi viwili tofauti.

Advertisement

Acheza winga, atesa kwa mabao

Wakati baba yake na babu yake wakitamba katika nafasi ya ulinzi, Daniel amechukua mkondo tofauti wa kucheza kama winga. Cesare alikuwa mlinzi imara aliyesifika zaidi kwa kucheza mipira ya juu huku Paolo akijulikana kwa kutumia akili nyingi na kutumia miguu yote miwili vema.

Paolo pia alikuwa akisifika kwa kucheza nafasi nyingi tofauti lakini Daniel ameamua kuchukua mkondo mwingine kwa kucheza winga ya kushoto. Msimu wa 2017/18 alifunga mabao 13 katika mechi 28 katika kikosi cha chini ya umri wa miaka 17.

Kiwango chake kilisababisha apelekwe katika kikosi cha chini ya umri wa miaka 19 msimu uliofuata. Katika kikosi hicho aliendeleza makali baada ya kufunga mabao 10 katika mechi 26. Mabao yote haya aliyafunga huku akicheza kama winga.

Hata hivyo bado Daniel ana kazi ngumu ya kupata nafasi katika kikosi cha kocha mpya wa Milan, Stefano Pioli kufuatia kufukuzwa kwa kocha wa zamani, Marco Giampaolo. Kikosi cha sasa cha Milan licha ya kusuasua lakini kina mastaa wanaotamba katika nafasi yake kama vile Hakan Calhanoglu, Fabio Borini, Suso, na Samu Castillejo.

Mapema wiki iliyopita Daniel alisaini mkataba mpya wa kuitumikia Milan mpaka mwaka 2024. Alipigwa picha akisaini mkataba huo mbele ya baba yake Paolo, bosi mtendaji wa Milan, Ivan Gazidis na Mkurugenzi wa ufundi wa Milan, Ricky Massara.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Italia vinadai kwamba karibu klabu zote 20 za Ligi daraja la kwanza nchini Italia maarufu kama Serie B zilikuwa zinamtaka kwa mkopo kinda huyo lakini inadaiwa kwamba Milan hawana mpango huo na wanataka kumuweka karibu na kikosi cha kwanza.

Atesa timu ya vijana ya Italia

Daniel tayari yupo katika vikosi vya vijana vya timu ya taifa ya Italia ambapo mwaka huu ameonyesha makali katika kikosi cha timu ya taifa ya Italia chini ya umri wa miaka 18 akicheza katika mechi dhidi ya Hungary na Uholanzi.

Baba yake ambaye alitwaa kombe la dunia na Italia mwaka 2006 nchini Ujerumani ni mmoja kati ya wachezaji walioacha alama kubwa katika soka la Italia ambapo alistaafu akiwa ameichezea mechi 126. Babu yake Cesare aliichezea timu ya taifa ya Italia mechi 14.

Familia nyingine zenye kizazi cha tatu

Familia ya Maldini sio ya kwanza kuwa na vizazi vitatu vilivyotamba katika soka. Miongoni mwa vizazi ambavyo babu, baba na mjukuu walitamba katika soka ni pamoja na familia ya mlinzi wa kushoto wa Chelsea, Marcos Alonso.

Baba yake Alonso, Marcus Alonso Pena alitamba katika vikosi vya Atletico Madrid na Barcelona na alitwaa taji la La Liga na Barcelona mwaka 1985, kabla ya hapo, baba yake Marcus Alonson Pena, Marquitos ambaye ni babu wa Marcos Alonso alitamba vilivyo na Real Madrid ambapo aloitwaa mataji matano ya Ulaya na wababe hao wa Santiago Bernabeu.

Staa wa zamani wa Manchester United, Diego Forlan naye alikuwa na kizazi kama hiki. Forlan ambaye alitamba zaidi Hispania huku pia akitwaa kiatu cha dhahabu katika fainali za kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini baba yake, Pablo aliwahi pia kuichezea Uruguay katika fainali mbili za kombe la dunia.

Lakini kabla ya hapo, baba yake Pablo ambaye ni babu yake Forlan, Juan Carlos Corazzo naye aliwahi kuichezea timu ya taifa ya Uruguay na kisha kuja kuwa kocha wao.

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...