Na Amiri kilagalila-Njombe
Wananchi na wakristu wa makanisa mbalimbali katika kata ya Mavanga wilayani Ludewa mkoani Njombe,wameungana na kupeana semina ili kupinga mila potofu ambazo zimekuwa zikifanywa na baadhi ya familia katika vijiji vya kata hiyo.
Akizungumza katika kongamano lililowakutanisha wanaume wa kata hiyo mara baada ya kukamilika kwa kongamano la vijana na wanawake yaliyofanyika katika kanisa katoliki, Paroko wa parokia ya Mavanga Padre Method Msanga amesema katika mazingira ya Mavanga kuna tatizo kubwa la imani potofu zinazopelekea watu kuchukiana.
“Tatizo kubwa tuliloliona ni watu kukata tamaa hasa vijana kwasababu hawaioni imani ya Mungu na badala yake wanaiona imani hiyo nyingine ya mila potofu na ya kishirikina hivyo tunataka tuamshe mioyo ya watu tufuate imani ya kweli na mwishoni tusiwe na hofu yoyote wala woga kwasababu Mungu yupo na baadaye tupate maendeleo”alisema Padre Method Msanga
Faraja Mapunda ni mchungaji wa kanisa la Anglican anasema wapo waumini wengi hawafiki makanisani kutokana na miungu mingine wanayoabudu kijijini hapo, kwa kuitolea sadaka wakiamini miungu hiyo inawasaidia kuwapa utajiri na wengine wakiamini inawaletea mvua kitu ambacho sio kweli.
“Kwa mfano kwenye vijiji vyetu mtoto wa kiume ambaye ni wa kwanza kuzaliwa wanasema lazima afanyiwe mila na wao wanaamini kwamba akifanyiwa hivyo anakuwa mtawala lakini imani nyingine wanasema anaongezewa nguvu katika sehemu za kiume kutokana na hayo madawa wanayomfanyia huko porini huku wazazi na mtoto akiwa uchi”alisema mchungaji Faraja Mapunda
![]() |
| Faraja Mapunda mchungaji wa kanisa la Anglican |
Joyce Mtweve ni mmoja wa wakazi wa kata hiyo aliyewahi kufanyiwa mila akiwa na umri mdogo wa miaka 16 baada ya kupata mtoto wa kwanza wa kiume,anasema alijiskia vibaya kutokana na yale aliyokutana nayo msituni huku akiwa uchi,kwani hata hivyo haoni faida ya kuendeleza mila hizo kwa kuwa hakuna utofauti na watoto wasiopitia mila.
Viongozi wa serikali hawako mbali katika kuungana na wananchi hao walioungana kupinga mila potofu ambapo Hakim Katabazi ni afisa mtendaji wa kata ya Mavanga,anasema mila potofu katika jamii yake imechangia kwa kiasi kikubwa katika kudidimiza shughuli za uchumi,huku kwa wiki akipokea kesi tatu mpaka nne zinazotokana na mila potofu.
“Kimsingi lazima tuondokane na hizi mila potofu kwasababu kwa ujumla wake zinachangia kabisa kudidimiza shughuli za kiuchumi,na hata leo nimekutana na kesi ya mama na baba wamekuja kulalamika kutokana na kesi hizi lakini,kwa wiki naweza kupokea tatu mpaka nne zinazotokana mambo ya imani potofu,na kesi nyingine wanamalizana wananchi huko huko mitaani”alisema afisa mtendaji
![]() |
| Joyce Mtweve mmoja wa wakazi wa kijiji cha Mavanga |
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsele amesema suala la imani potofu katika wilaya hiyo ni kubwa hali ambayo imeendelea kuleta madhara makubwa kuuanana wengine kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi.
“Janga kubwa la hapa Ludewa ni imani potofu ya ushirikina na uchawi, na jambo hili limesababisha watu kutoamini kwamba mtu akiumwa anaweza akatibiwa hospitalini na akifa atakuwa amekufa kwa ugonjwa na baadaye visa vikubwa na kuuana, na jambo hili la ushirikina pia limesababisha kuenea kwa kiwango kikubwa sana kwa maradhi ya ukimwi”alisema Andrea Tsele
![]() |
| Paroko wa parokia ya Mavanga wilayani Ludewa Padre Method Msanga |




No comments:
Post a Comment