Search This Blog
Wednesday, October 2, 2019
Naibu Waziri ataka watu wenye Ulemavu wajumuishwe katika masuala ya Ukimwi
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masula ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa ameuasa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kushirikisha kundi la wenye ulemavu katika masuala ya UKIMWI ili kuhakikisha jamii nzima inapata elimu na huduma ya masuala hayo.
Ametoa kauli hiyowakati alipokuwa akizungumza na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo mkoani Tanga alipofanya ziara yake ya siku tatu mkoani hapo ili kutembelea na kukagua shughuli zinazotekelezwa wilayani hapo kuhusu masuala ya UKIMWI.
Alieleza kuwa kundi la wenye ulemavu limekuwa nyuma kwa muda mrefu katika kujumuishwa hususan katika masuala ya elimu na huduma za kijamii hivyo ni lazima kuzingatia mahitaji yao katika kuendelea kuwapa elimu na huduma za masuala hayo ili waweze kunufaika na huduma ili kupunguza na kuondoa maambukizi mapya katika mkoa mzima wa Tanga.
“Ni vyema kuhusisha kundi la wenye ulemavu katika upatikanaji wa huduma za masuala ya Ukimwi kwa kuzingatia kundi hili limekuwa likisahaurika na kutofikiwa kama yalivyo makundi mengine,”alieleza Mhe.Ikupa
Aliongezea kuwa miongoni mwa mikakati ya Halmashauri ni vyema kuwa na mipango madhubuti ya kuhakikisha huduma za masuala ya Ukimwi ikiwemo, utoaji elimu juu ya mabadiliko ya tabia na kinga dhidi ya maambukizi ya VVU, kuwashirikisha katika program mbalimbali zinazojikita katika kuimarisha mifumo utoaji wa elimu ya masuala ya watu wanaoishi na VVU na mikakati ya kusaidia makundi hayo.
Alifafanua kuwa, kwa kufanya hivyo itasaidia kupungua kwa masuala ya ubaguzi katika jamii ili kuwa na usawa na haki kwani wenye ulemavu wanastahili kupewa huduma sawa katika jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Mwanashaa Rajab alieleza kuwa wameendelea kuwafikia watu wenye ulemavu katika huduma za upimaji, utoaji wa huduma za dawa na kuahidi kuendelea kuwajumusha katika shughuli zote zinazohusu masuala ya ukimwi ili kufikia malengo ya Taifa ya kuwa na tisini tatu (909090).
“Tunakushukuru kwa kuendelea kuunga mkono jitihada zetu na kukuahidi tutatekeleza maagizo yako ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti zinazojumuisha mahitaji maalum ya wenye ulemavu, kuwapatia elimu, kuwafikia na kuendelea kuwashirikisha katika program mbalimbali za kimaendeleo,”alisema Mwanashaa.
Naye Mratibu wa Kudhibiti masula ya Ukimwi katika Halmashauri hiyo Herieth Nyangasa alieleza kuwa hali ya maambukizi kipindi cha mwaka 2018 ni asilimia 2.1 kutoka asilimia 2.6 kwa mwaka 2017 ambapo imechangiwa na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuwafikiwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi ili kuhakikisha maambukizi mapya yanapungua.
“Zipo jitihada nyingi zimefanyika kuhakikisha wanapunguza hali ya maambukizi mapya na kuwapatia huduma watu wanaoishi na VVU ikiwa ni pamoja na wilaya kuwa na vituo 445 vya kutolea huduma ya ushauri nasihi na upimaji wa VVU, vituo 20 vya upimaji kwa hiari, vituo 38 upimaji kwa ushawishi na vituo 45 vya huduma ya kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,”Alesema Nyangasa
Kwa upande wake Mratibu wa kudhibiti Ukimwi Wilayani humo Dkt. Yahaya Mbura alieleza changamoto zinazokwamisha jitihada za serikali katika kuwahudumia watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kuwa ni pamoja na tatizo la utoro wa watumiaji wa dawa za kufubaza Virusi vya ukimwi ambapo alieleza imechangia kwa kikasi kikubwa kudhoofisha jitihada hizo.
“Hadi sasa tuna ripoti za utoro kwa wanaotumia dawa wapatao 388 na hii imechangiwa na changamto za miundombinu kipindi cha mvua, umbali wa vituo kutoka katika makazi yao pamoja na uwepo wa imani potofu kuhusu matumizi ya dawa hizo,”alisisitiza Dkt. Yahaya.
Aliongezea kuwa pamoja na changamoto hiyo, tayari zaidi ya watoro 212 walifanikiwa kuwarejesha katika huduma za upatiwaji wa dawa na kuendelea kutumia dawa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Punguza kilo tano kwa siku saba
NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...
-
Kiwanja kinauzwa kipo Dodoma Mahungu njia ya kwenda Singida kabala hujafika NALA. Kiwanja ni cha Makazi kinaukubwa wa Sqm 450 ( 15 X...
-
Akionekana kwa mara ya kwanza kwa umma tangu aondoke madarakani, aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameweka wazi uwezekano wa kuwania...

No comments:
Post a Comment