Search This Blog

Sunday, September 29, 2019

TPB yazindua tawi jipya Masasi


Na Ahmad Mmow, Lindi

Benki ya Posta Tanzania( TPB) imefungua tawi lake dogo jipya wilayani Masasi Mkoani Mtwara ili kutimiza dhamira ya benki hiyo ya kupeleka huduma za kibenki karibu zaidi na wananchi,hasa wale wanaoishi maeneo ya wilayani na vijijini katika mikoa ya kusini.

Hafla ya uzinduzi wa tawi hilo jipya wilayani Masasi imefanyika jana wilayani hapo katika viwanja vya tawi la benki hiyo mpya maarufu kama mkuti mjini Masasi na kuhudhuliwa na wadau mbalimbali.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo kufanyika mtendaji kuu wa benki hiyo (CEO) Sabasaba Mongishi alisema kuwa wameamua kusongeza huduma za benki ya Tpb kwa wananchi wa wilaya ya Masasi.

Alisema kwa muda mrefu wakazi wa wilaya hiyo na wilaya za jirani wamekuwa na kiu kubwa ya kupata huduma ya benki ya Posta Tanzania hivyo hitaji hilo sasa limepatiwa jawabu kwa kufungua tawi hilo jipya Masasi.

Alisema tangu ianzishwe mwaka 1925 na sasa kutimiza miaka 94 imekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuongeza idadi ya matawi kutoka matawi 32 hadi kufikia matawi 77.

Alisema benki ya TPB imeendelea kutoa gawio kwa wanahisa wake ikiwemo mwanahisa wake namba moja ambaye ni serikali.

Mongishi alisema  kwa mwaka 2019 benki hiyo tayari imeshatoa gawio la sh.bilioni 1.2 kwa wanahisa wake ikiwemo serikali ambaye ni mwanahisa namba moja.

Alisema kabla ya mabadiliko ya benki hiyo ilikuwa ikitengeneza faida chini ya sh.bilioni 1 lakini kwa mwaka 2018 Tpb benki imetengeneza faida ya sh.bilioni 17.2 na mwaka 2017 ilitengeneza faida ya sh.bilioni 18.

Mongishi alisema mwaka huu benki hiyo imejipanga kupata faida ya zaidi ya sh.bilioni 20 na kwamba itawafikia wateja wake mpaka maeneo ya vijijini hususani kuwafikia wakulima wa korosho.

Mongishi aliwaomba wafanyabiashara na wateja kwa ujumla kutumia fursa ya uwepo wa tawi hilo kupata huduma zote za kibenki zinazotolewa na benki hiyo mbazo ni sawa zinazotolewa kwenye matawi mengine ya benki ya Tpb nchini.

 "TPB benki imepanua wigo zaidi katika utoaji huduma za kibeki ngazi za chini kwani hadi sasa ni asilimia 17 pekee ya watanzania ndio wenye akaunti benki hivyo kufungua tawi hili hapa Masasi itakuwa tumewasogolea wananchi," alisema Mongishi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Mtwara, Gelasius Byakanwa ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo, alizitaka benki zote mkoani humo zitoe huduma bila ya kuwataka wateja kutoa rushwa.

Aidha, Byakanwa aliwataka maofisa mikopo wa taasisi za kibenki kufanya kazi kwa uweledi ili wasiwe chanzo cha upotevu wa fedha kwenye ofisi zao,pia elimu ya mikopo itolewe hasa kwa wakulima.

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...