Search This Blog

Tuesday, September 3, 2019

Serikali kufanya mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Kilimo


Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema kuwa serikali ya Tanzania imejipanga kuikabili sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuona umuhimu wa kuwaandaa watanzania katika kubadilisha kilimo chao kutoka kwenye kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara.

Waziri Hasunga ameyasema hayo wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima katika Ofisi za Ubalozi huo zilizopo katika mtaa wa 12, Abba Hillel Silver Jijini Tel Aviv nchini Israel.

Alisema kuwa katika ziara yake hiyo amejifunza namna ambavyo nchi ya Israel imepiga hatua ya ujuzi katika sekta ya kilimo hivyo kuona umuhimu wa serikali ya Tanzania kuwekeza katika skimu za umwagiliaji.

Alisema kuwa asilimia kubwa ya wakulima nchini Tanzania wanatumia majembe ya mkono katika kilimo jambo ambalo haliwezi kuongeza tija na uzalishaji. “Tunatumia majembe ya mkono mbaya zaidi kilimo chetu kinategemea msimu wa mvua, hivyo kilimo cha namna hiyo bado kinatuchelewesha,tuna wajibu wa kujifunza kwa wenzetu walioendelea” Alisema Mhe Hasunga

Alisema kwa kuanza serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa kilimo inaweza kujenga mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uwezo wa kilimo cha umwagiliaji kitakachofanya kazi msimu mzima badala ya kilimo cha kutegemea mvua.

Hasunga alisema kuwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kadhalika wizara ya Viwanda na Biashara zitafanya kazi kwa pamoja ili kuona namna ya kuzalisha kwa tija mazao ya kilimo na kutoa malighafi nyingi zitakazochangia katika kuinua na kuchagiza matakwa ya serikali ya kuwa na serikali ya viwanda.

Kuhusu masoko ya mazao yanayozalishwa nchini Tanzania Hasunga alisema kuwa serikali inaendelea na mkakati maalumu wa kuimarisha masoko kwani imeanzisha kitengo maalumu katika wizara ya kilimo kitakachokuwa na wajibu wa kushughulikia masoko ya mazao ya wakulima.

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga ameyaalika makampuni mbalimbali ya Israel yanayojishughulisha na kilimo kutembelea nchini Tanzania kwa ajili ya kujionea fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania.

“Tanzania ni nchi yenye rutuba nzuri, eneo kubwa kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo, hivyo nayaalika makampuni yote yanayohusika na kilimo hususani yanayojishughulisha na utafiti, kutembelea Tanzania kwani ni nchi yenye eneo zuri na kubwa kwa ajili ya uwekezaji hususani katika sekta ya kilimo” Alikaririwa Hasunga

Hasunga amesema kuwa Israel ni nchi yenye eneo dogo kwa ajili ya kilimo lakini wanazalisha chakula kinachotosheleza wananchi wake sambamba na kuuza mazao yao nje ya nchi jambo ambalo linaimarisha pato la serikali ya nchi hiyo na kipato cha mtu mmoja mmoja.




No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...