Search This Blog
Tuesday, July 23, 2019
Waziri Mkuu azionya halmashauri zilizolega makusanyo ya kodi
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezionya Halmashauri za Wilaya na Manispaa zilizoshindwa kufikisha malengo ya makusanyo ya kodi na kuzitaka zijitathmini ni kwa nini hazijafikisha malengo hayo.
“Kuna Halmashauri zimetajwa hapa kwamba hazijafikisha malengo ya makusanyo ya ndani. Fanyeni tathmini, ni kwa nini hamjafikia malengo na mhakikishe kuwa mwakani hamji kutajwa tena kwenye mkutano kama huu,” alisema. Halmashauri hizo ni Kakonko, Buhigwe, Madaba, Kigoma, Momba na Songea.
Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na washiriki wapatao 700 ambao ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) unaoendelea jijini Mwanza.
Waziri Mkuu ambaye amefungua mkutano huo wa siku tatu kwa niaba ya Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, amewataka washiriki wa mkutano ambao ni Mameya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Majiji, Miji na Manispaa, wasimamie makusanyo ya mapato kupitia vyanzo vyao ili waweze kupanga mipango ya maendeleo. “Lengo la Serikali ni kuwezesha kila Halmashauri zijitegemee kwa asilimia 80-100 ifikapo 2025,” amesema.
“Katika makusanyo hayo, hakikisheni kuwa mnatenga asilimia 40 kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Na hili ni tatizo kwa Halmashauri nyingi zikiwemo zile kubwa. Ukifuatilia kwa makini huoni miradi inayogusa maisha ya wananchi wa kawaida.”
“Ukichukulia Dar es Salaam au Arusha ambao wanakusanya kati ya shilingi bilioni tano na 10, ni mradi gani wa thamani kubwa uliojengwa kwa kutumia fedha zenu za ndani, ukiacha hii mikubwa ya stendi za mabasi au barabara za lami ambayo inajengwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu?” alihoji.
“Hivi kuna Halmashauri ambayo imejenga kituo cha afya cha kisasa kwa kutumia fedha zake za makusanyo? Afadhali hawa wa Dodoma ambao wameanza kujenga stendi ya mabasi na hoteli mbili za kitega uchumi,” amesema.
“Uamuzi wa Mheshimiwa Rais Magufuli wa kukusanya fedha zote na kuziweka kwenye chanzo kimoja ulitokana na study ya muda mrefu iliyofanyika na kubaini kuwa fedha zinazokusanywa haziendi kwenye miradi inayogusa wananchi. Niwasihi sana, fanyeni miradi ambayo kila Mtanzania angependa kuiona kwenye Mamlaka zenu za Serikali za Mitaa,” amesisitiza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Punguza kilo tano kwa siku saba
NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...
-
Kiwanja kinauzwa kipo Dodoma Mahungu njia ya kwenda Singida kabala hujafika NALA. Kiwanja ni cha Makazi kinaukubwa wa Sqm 450 ( 15 X...
-
Akionekana kwa mara ya kwanza kwa umma tangu aondoke madarakani, aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameweka wazi uwezekano wa kuwania...

No comments:
Post a Comment