Search This Blog

Monday, July 22, 2019

Waziri Mkuu aagiza eneo la mnara wa Zinjathropous kuboreshwa


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii isimamie uboreshaji wa eneo la mnara wa Zinjathropus ili paweze kuvutia zaidi.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi na viongozi waliohudhuria maadhimisho ya miaka 60 ya kumbukizi ya ugunduzi wa fuvu la Zinjathropus Bosei, eneo la bonde la Olduvai, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha.

Maadhimisho hayo yamefanyika ndani ya hifadhi ya Ngorongoro sambamba na uzinduzi wa makumbusho ya Dkt. Mary Leakey. Mnara wa Zinjathropus na Homo habilis umejengwa kwenye hifadhi ya Ngorongoro karibu na njia panda ya kuelekea bonde la Olduvai.

“Kwenye mnara wa Zinjathropus na Homo habilis pasiachwe kama palivyo. Pajengwe seng’eng’e kuzunguka eneo lile lakini pia paweke kibanda cha mlinzi ambaye pia atakuwa anatoa taarifa kwa wageni wanaopita hapo.”

“Mtafute vijana kadhaa ambao ni wenyeji wa eneo hili, wafundishwe historia kamili kisha wapewe ajira hizo. Kibanda kikijengwa kwa juu kiwe na vioo ili anayelinda aweze kuona pande zote na pia muweze kumkinga na vumbi na upepo mkali wa eneo lile.”

Waziri Mkuu pia alitembelea korongo la Frida Leakey, (mahali ambapo zinjathropous aligunduliwa) na kupata maelezo juu ya kugunduliwa kwa fuvu la mtu wa kale duniani yapata miaka milioni mbili iliyopita.

Akigusia kuhusu uhifadhi wa eneo hilo, Waziri Mkuu alisema nako pia pajengwe kibanda cha mlinzi mwenye uwezo wa kutoa taarifa kwa watalii na akasisitiza pia ajira hizo ziwahusu wenyeji wa eneo hilo.

“Kwenye korongo la Frida, pawekwe bango lenye maelezo ya Kiswahili, nako pia wapatikane vijana sita au nane, waeleweshwe hiyo historia, wakifuzu, Wizara iwawezeshe, wapangiane zamu ya kushinda hapo. Pia pajengwe kibanda cha wageni kupumzikia wakifika eneo hilo.

Kuhusu makumbusho ya Dkt. Leakey, Waziri Mkuu alisema makumbusho hayo ni lulu kwa Taifa. “Ninawapongeza viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Ngorongoro kwa kuendeleza na kutunza makumbusho haya.”

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangallah alisema kwa sasa dunia inatambua kuwa chimbuko la binadamu ni Afrika. “Hata kama tunatofautiana sura na rangi, watu wote duniani wana asili ya Afrika. “Kwetu sisi Tanzania, tunaadhimisha uvumbuzi huu kwa sababu fuvu la Zinjanthropus ni alama na nembo ya Tanzania na dunia.”

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...