Search This Blog

Wednesday, June 12, 2019

Wananchi wapambana kukamilisha vyumba vya madarasa


Na Amiri kilagalila, Njombe

Wananchi wa Kata ya Igongolo Halmashauri ya wilaya ya Njombe mkoani Njombe, Wameendelea kushiriki Ujenzi wa vyumba vinne vya Madarasa kwaajili ya Matumizi ya Wanafunzi wa Kidato cha tano na Kidato cha Sita katika shule ya Sekondari Ipitingi ambayo ni shule ya Kata hiyo.

Diwani wa Kata ya Igongolo , Isaya Muyamba amesema kuwa Shule hiyo iliyojengwa katika Kijiji cha Itipingi ipo chini ya Wananchi wa Kata ya Igongolo ilianza rasmi Mwaka 2003 ikiwa na Kidato cha kwanza hadi kidato cha nne na mwaka 2017 Serikali ilitoa kibali cha kuanzisha kidato cha Tano shuleni hapo.

Amesema kuwa licha ya kupata kibali cha kuanzisha kidato cha Tano na cha Sita, Shule ya Sekondari Itipingi bado inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya Madarasa kwaajili ya kusomea Wanafunzi wa vidato hivyo hali iliyowalazimu Viongozi kwa kushirikiana na Wananchi wa Kata ya Igongolo kuanza mchakato wa Ujenzi wa vyumba vinne vya Madarasa.

“Awali kabla ya kuwa na Kidato cha tano na cha Sita, Shule hii ilikuwa haina upungufu kabisa wa Vyumba vya madarasa lakini tulipopata bahati ya kuwa na vidato hivi tukajikuta tuna upungufu wa vyumba vya madarasa, Tayari tumeanza hatua za kutatua changamoto hii” Amesema mh. Isaya Muyamba Diwani wa kata ya Igongolo.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Madarasa hayo ambae pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Itipingi Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Bw, Adriano Mtwigu, amesema kuwa Ujenzi wa Vyumba vinne vya madarasa umeanza kwakutumia nguvu za Wananchi wa kata ya Igongolo ambao wanatoa kiasi cha Tsh, 10,000/= kila mmoja ili kufanikisha zoezi hilo.

Ameongeza kuwa kamati ya Ujenzi imekubaliana kufanya Harambee Julai 27/2019 ambayo itawakutanisha Wananchi wa vijiji vyote vya Kata ya Igongolo, Wazawa wa kata hiyo wanaoishi nje ya kata pamoja na Wadau mbalimbali wa Maendeleo kutoka ndani nan je ya Kata ya Igongolo ambao wanapenda kuunga mkono Juhudi za Wananchi wa kata hiyo.

“Tutafanya Harambee kubwa tarehe 27/07/2019 ili kuchangia ujenzi wa Vyumba Vinne vya madarasa ambayo baada ya kukamilika yatatumika kwaajili ya Wanafunzi wa Kidato cha tano na Kidato cha Sita hapa Shuleni” Ameeleza Bw, Adriano Mtwigu, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...