Spika wa bunge la Libya aidhinisha uchaguzi wa Disemba
Spika wa bunge la Libya lenye makao yake upande wa mashariki amesaini sheria inayoruhusu uchaguzi wa rais kufanyika mwezi Disemba mwaka huu, ingawa muhimili mwengine wa dola umeiita sheria hiyo kuwa imepotoka. Spika Aguilah Saleh ameituma sheria hiyo inayoamuru kufanyika uchaguzi tarehe 24 Disemba kwa vyombo vyengine vya kisiasa pamoja na Umoja wa Mataifa, kwa mujibu wa msemaji wa bunge hilo.
Baraza Kuu la Dola, ambalo limepewa nguvu na muafaka wa kisiasa wa 2015, limesema Spika Saleh aliipitisha sheria hiyo peke yake kwa madaraka asiyokuwa nayo, kwa lengo la 'kuukwamisha uchaguzi ujao kwa kutoa makusudi sheria isiyofaa.'
Kufanyika kwa uchaguzi wa rais na wabunge ni moja ya masharti ya makubaliano ya kisiasa yaliyodhaminiwa na Umoja wa Mataifa na yaliyoanzisha serikali ya umoja wa kitaifa mwezi Machi.

No comments:
Post a Comment