Kikosi cha mauaji kinachoundwa na askari wengi wastaafu wa Colombia kinatajwa kuhusika katika mauaji ya Rais wa Haiti, Jovenel Moise, yaliyotokea wiki hii, Polisi imesema.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Haiti, Leon Charles, kikundi hicho kinajumuisha raia 26 wa Colombia na wamarekani wawili weye asili ya Haiti.
Mpaka sasa, watuhumiwa 17 wameshakamatwa wakiwemo wamarekani hao, huku wengine nane wakiendelea kusakwa. Washukiwa wengine kadhaa waliuawa kwa risasi katika mapambano na Polisi katika mji mkuu wa Port-au-Prince.
Mapema Jumatano kundi kubwa la watu waliokuwa na silaha walivamia makazi binafsi ya Rais na kuanza kushambulia. Mke wa Rais Moise, Martine alijeruhiwa katika mashambulizi hayo na kukimbizwa Florida, Marekani kwa matibabu, na inaelezwa anaendelea vizuri.
Haijafahamika mara moja nani aliye nyuma ya mipango ya mauaji ya kiongozi huyo na kwa lengo gani.
Ingawa Waziri mkuu wa mpito wa Haiti, Claude Joseph, ambaye anaongoza nchi hiyo kwa sasa ameiambia BBC kwamba Rais huyo mwenye umri wa miaka 53 alikuwa anakabiliana na aliowaita manguli wenye ushawishi mkubwa nchini humo.

No comments:
Post a Comment