Klabu ya Manchester City imeshinda kwa mara ya tatu ligi ya Premia kwa miaka minne mfululizo baada ya washindani wake wa karibu Manchester United kufungwa na Leicester City jana usiku.
Kikosi hicho kinachonolewa na Pep Guardiola sasa kina alama 10 zaidi ya United ambao wapo nafasi ya pili huku wakiwa wamebakiwa na michezo mitatu peke yake.
Hii ni mara ya saba kwa City kushinda ubingwa wa England, na ni ubingwa wao wa tano ndani ya miaka tisa.
"Huu umekuwa msimu wa kipekee kabisa wa kuchukua taji la Ligi ya Primia (EPL)," alisema Guardiola.
"Msimu huu ulikuwa mgumu. Tutaukumbuka daima msimu huu na jinsi tulivyoshinda. Ninajivunia kuwa meneja hapa na katika kundi la wachezaji hawa.
"Ni wachezaji wakipekee sana. Kushinda katika msimu huu, kukiwa na marufuku nyingi na changamoto tulizokabiliana nazo lakini bado tukaendelea kufanya vizuri - ni jambo kubwa sana.
"Kila siku , wapo kwenye mapambano ya kufanikiwa, kujaribu kila siku kuwa bora zaidi. Tumekuwa mashujaa.
"Nilikuwa Uhispania, nikawa Ujerumani na ninaweza kusema mpaka sasa kuwa hii ndio ligi ngumu. Hivyo ligi hii ina maana kubwa kwa kila mmoja."
Guardiola, mwenye miaka 50, ameshinda mataji nane ya ndani tangu ajiunge na Manchester City mwaka 2016.
City ilikuwa na mwanya wa kushinda taji la EPL siku ya Jumamosi lakini ilifungwa na Chelsea kwa magoli 2-1.
Hata hivyo, Leicester wameimaliza kazi yao kwa kuifunga Man United magoli 2-1 katika uwanja wao wa Old Trafford siku ya Jumanne.
Ni ubingwa wa sita ambao umeamuliwa kwenye uga wa Old Trafford - ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuliko uwanja mwengine wowote - na kati ya mara hizo sita United imenyakua ubingwa mara tatu na mara tatu zilizosalia ukienda kwengine, ikiwemo msimu huu.
Huu ni ubingwa wa pili kwa City ndani ya kipindi cha wiki mbili baada ya kuifunga Tottenham katika fainali ya kombe la Carabao. City pia wameingia katika fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya kuwafunga mabingwa wa Ufaransa Paris St-Germain wiki iliyopita.
Tangu iliponunuliwa na matajiri kutoka Abu Dhabi mwaka 2008, City imeshanyakua makombe 12.
Wanatarajia kupatiwa kombe lao katika mechi ya mwisho dhidi ya Everton Mei 23, mbele ya mashabiki 10,000.

No comments:
Post a Comment