Serikali ya Djibouti imesema leo kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Omar Guelleh ameshinda kwa kishindo muhula wa tano madarakani kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika siku ya Ijumaa.
Akinukuu matokeo ya awali ya uchaguzi huo waziri wa mambo ya ndani ya Djibouti Mumin Ahmed amewaambia waandishi habari kuwa Guelleh amepata ushindi wa asilimia 98 akimshinda mpinzani wake mkuu Zakaria Farah.
Ingawa matokeo rasmi yanatarijiwa kutangazwa baadae leo, rais Guelleh ametumia ukurasa wake wa Twitter kuwashukuru wapiga kura kwa imani waliyomuonesha na amewatolea wito wa kuendelea kufanya kazi pamoja.
Mgombea wa upinzani Zakaria Farah ambaye alisitisha kampeni zake mapema kutokana na wasiwasi wa usalama hajazungumza chochote kuhusiana na taarifa hizo za matokeo ya uchaguzi.
Vyama vingine vya upinzani vilisusia uchaguzi huo ambao baadhi ya asasi za kiraia zimesema umekosa uhalali.

No comments:
Post a Comment