Ziara rasmi ya Ufaransa iliyotekelezwa na Rais wa Misri Abdulfattah al-Sisi mnamo Desemba 7, imepingwa kwenye maandamano yaliyoandaliwa katika mji mkuu wa Paris.
Umati wa watu uliokusanyika mbele ya jengo la Bunge, ulipinga vikali hatua ya Rais Emmanuel Macron ya kumkaribisha al-Sisi kwa zulia jekundu katika Ikulu ya Elysee.
Maandamano hayo yaliyohudhuriwa na wawakilishi wengi wa mashirika ya kimataifa ya haki za kibinadamu, wabunge wa Jumuiya ya Ulaya na wanachama wa upinzani wa Ufaransa, pia yalimpinga Macron kumkaribisha al-Sisi kwa lengo la kutaka kuuza silaha, na kumtaja kama dikteta aliyeingia madarakani kwa njia ya mapinduzi.
Wawakilishi wa mashirika ya haki za kibinadamu walikumbushia maelfu ya watu wasio na hatia na waandishi wa habari wanaoshikiliwa katika magereza ya Misri, na kuhimiza jamii ya kimataifa kushinikiza utawala wa al-Sisi kuwaachilia huru wafungwa hao.
Waandamanaji hao ambao walioelezea mapokezi ya al-Sisi kwenye zulia jekundu kuwa kama mapokezi ya "dikteta mwenye damu", pia walishutumu vyombo vya habari vya Ufaransa kwa kukaa kimya.
Jumuiya ya kimataifa na watetezi wa haki za kibinadamu waliwahi kupinga "kukaribishwa kwa dikteta kama al-Sisi nchini Ufaransa, ambapo ni suala lisilohusiana na uhuru."

No comments:
Post a Comment