Search This Blog

Monday, February 17, 2020

Koba, asimulia kilichompata kwa Nassor Michael ulingoni

By Imani Makongoro

Licha ya kustaafu ngumi mwishoni mwa miaka ya 1990 bado kiwango cha Koba Kimanga hakijasahaulika kwa wadau wa ngumi nchini mpaka sasa.

Bondia huyo bingwa wa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1995 kwenye uzani wa super middle anaeleza namna alivyoanza ngumi kama ‘deiwaka’.

“Nilikuwa naenda Relwe Gerezani kuangalia mazoezi sikuwa na uelewa na ngumi kaka yangu (Hamisi) ndiye alikuwa akijifua pale mwaka 1978 wakiwa na kocha Habibu Kinyogoli ‘Master,” anasimulia.

Pamoja na kucheza mapambano mengi yakiwemo ya kimataifa, Koba anasema hatamsahau mbabe wa zamani wa ngumi Nassor Michael ambaye baadaye alikuwa kocha wa timu ya taifa.

Koba anasema pambano lake na Nassor lilikuwa gumu na alitamani kukimbia ulingoni kutokana na makonde aliyomiminiwa na mbabe huyo.

Nassor anasema pambano hilo lilipigwa mwaka 1983 na lilivuta hisia za mashabiki wengi kutokana na umaarufu wa mpinzani wake huku yeye (Koba) akiwa bondia chipukizi anayeinukia.

Advertisement

Pambano lenyewe

“Niliingia ukumbini niko hovyo wakati ule hata jezi na ring bout (raba za ulingoni) sikuwa nazo nilipomuona Nassor anapasha na kapendeza, nikaona kuna dalili zote za kupigwa.

“Ilikuwa bado kidogo nikimbie kama kocha wangu angenipa mwanya kidogo tu siku ile basi ningekimbia maana nililiogopa pambano baada ya kumuona Nassor yuko na muonekano wa kibondia mimi nikiwa nimevaa mavazi ya kiwango cha chini.

“Ngumi ya kwanza tu nikapelekwa chini, nikahesabiwa nikanyanyuka nikasema bado naendelea niko fiti, ngumi ya pili ikanikuta nikarudi chini, kocha Said Tambwe akaona nitakufa akarusha taulo ili kuniokoa.

“Nikalinyanyua lile taulo kwa mguu nikalirusha nje ya ulingo, nikasema naendelea ujasiri ule ukamuogopesha hata Nassor, nilikuwa na usongo kweli kweli licha ya kuanza vibaya.

Anasema raundi ya pili, Nassor akapunguza kasi, yeye (Koba) akaanza kumshambulia na ili kujilinda Nassor alianza kukumbatia.

“Nilipigwa kwa pointi za majaji 4-1 nilijiona nina kitu kwani kama jaji mmoja ameona nimeshinda basi mimi ni bondia wa kiwango bora, kocha wa timu ya Taifa ya ngumi wakati ule raia wa Bulgaria hakuniacha alinichukua kwenye kambi ya maandalizi ya Olimpiki.

Kambi ile iliwajumuisha mabondia nguli wakati huo, Lucas Msomba, Makoye Isangula na Nassor, ingawa Koba hakwenda kwenye Olimpiki.

Anasema miaka miwili baadaye, Nassor akaanza kuchoka na yeye Koba akaandaliwa kuwa mbadala wake katika ngumi za uzito wa juu.

Koba anasema hakutarajia kuwa bondia maarufu kwani alianza kujifunza ngumi kama kujifurahisha alipokuwa akisoma shule ya msingi alijifua kwa ajili ya kupambana na wanafunzi watukutu.

“Siku moja nikiwa nimepata uzoefu pale mazoezini nikapewa kufanya sparing (mazoezi ya ana kwa ana) na bondia anaitwa Kerenge Abdallah alinipiga sitakaa nisahau.

Anasema licha ya kipigo hicho hakujali kila alipopelekwa chini kwa makonde mazito ya mpinzani wake alinyanyuka na kuendelea na pambano.

“Kila mtu alishangaa umri wangu na namna nilivyopambana Kerenge mwenyewe hakuamini, baada ya pambano alimwambia kocha huyu dogo atakuja kuwa bondia mzuri akaze buti tu,” anasema Koba.

Klabu ya Simba yamtoa

Koba anasema baada ya sparing ile sifa zake zikaanza kuvuma, lakini wakati huo alikuwa bado kijana mdogo ndipo Kinyogoli ambaye alikuwa kocha wa ngumi wa klabu ya Simba akaamua kumchukua.

“Nikiwa Simba nilianza kubadilika na kuongeza kiwango nilijiona tofauti, tayari nilishamaliza shule na kuanza kucheza ngumi lakini sikuwa na jina (staa).

“Wakati ule staa wa ngumi alikuwa Nassoro Michael wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alikuwa akijiandaa na mashindano ya Afrika, hivyo nikaambiwa nisaidie katika sparing.

“Kipindi chote cha mazoezi, Nassor alikuwa akinipiga kama anapiga begi, lakini sianguki sio kama nilikuwa fiti nilivumilia ila nikitoka pale maumivu yake si ya mchezo.

Atwaa dhahabu

Koba anakumbuka pambano la kwanza alicheza na Hamisi Nindi kutafuta bingwa wa mkoa.

“Nindi wakati ule alikuwa yuko profesheno nilimpiga kwa pointi na kuwa bingwa wa mkoa kwenye uzani wa super middle.

Baada ya mashindano hayo ikatokea mashindano mengine ambayo Nassor naye alikuwa akicheza kutafuta timu ya maandalizi ya Olimpiki ya mwaka 1984.

“Nassor hakuwa na mpinzani nikaambiwa mimi nipigane naye siku napewa zile taarifa kwanza nilikataa, kocha akaniambia lazima nipigane, nitake nisitake tena kwa kupandisha uzani na kuchezea light heavy (kilo 81) kutoka super middle (kilo 76).

Ikumbukwe wakati huo, Nassor ambaye baadaye alikuja kuwa kocha wa timu ya Olimpiki ya mwaka 2008 alikuwa staa nchini.

Pambano lampa ajira Polisi

Mwaka 1986 Koba alipata ajira kwenye Jeshi la Polisi kutokana na kipaji chake cha ngumi.

Anasema alishawishiwa kuingia Polisi na mmoja rafiki yake ambaye wakati ule alikuwa ni mtumishi wa jeshi hilo.

“Aliniambia, Koba kwanini usiingie Polisi kwani una sifa zote ambazo Jeshi la Polisi linazihitaji, akanipeleka makao makuu, nikachukuliwa nikapelekwa CCP Moshi.

“Kule hatukupata ajira, tukawa tunacheza tu, siku moja likaandaliwa pambano kati yangu na Gulai, ambalo lilikuwa gumzo.

“IGP wa wakati ule alikuwa mgeni rasmi, si unajua ukiwa mchezaji, halafu bosi wako yuko uwanjani, utacheza kwa kiwango chako chote, ndivyo ilikuwa kwangu.

Anasema alimpiga Gulai kama begi, kuanzia hapo akawa maarufu katika timu ya Polisi na IGP akaruhusu waajiriwe na mwaka 1987 akaenda rasmi depo.

Ailetea nchi medali ya dhahabu

Mwaka 1995, Koba alitwaa medali ya dhahabu kwenye mashindano ya nchi za ukanda wa Afrika na Kusini mwa Afrika yalifanyika nchini Botswana.

“Nilikuwa bondia pekee wa Tanzania kutwaa medali katika mashindano hayo, ilikuwa faraja kwangu na nilipokelewa kama shujaa, aliyelipigania taifa na kupewa heshima ya kupandishwa cheo kazini.

Mabondia wa sasa wengi waoga

Koba anasema tofauti na miaka ya nyuma, mabondia wa kizazi cha sasa wengi ni waoga na baadhi yao wamekuwa wakiogopa au kuchagua wapinzani.

“Zamani hakukuwa na mambo hayo ndiyo sababu tulikuwa fiti ilikuwa bondia hadi uruhusu kupigwa KO mpinzani wako amefanya kazi kweli kweli.

“Nakumbuka mimi siku moja nilipigwa ngumi ikanikuta ikanichana mdomoni meno yakatoka nje, mdomo ukawa kama umekatwa katikati, lakini nilitaka kuendelea kupigana.

Anasema furaha yao ilikuwa ni kupigana, ukipigwa unaomba pambano la marudiano hadi ushinde.

“Mimi nilikuwa na rafiki yangu, naye alikuwa bondia aliitwa Steven ‘Biko’ Mwakasanga.

“Tulipigana naye nikampiga, hakukubali, tukaandaliwa marudiano nikampiga, ile ilimuuma mno hakukubali akaomba marudiano kwao Mbeya tulipigana hadi raundi zinakwisha si mimi wala yeye ambaye alijua kama raundi zimeisha akashinda kwa pointi.

Kiboko yake huyu hapa

Mbali na Nassor ambaye alimsumbua Koba ulingoni, bondia huyo anamtaja Wamboi Mangole.

“Huyu jamaa alikuwa ana nguvu za ajabu siku moja nilipigana naye Diamond Jubillee.

“Yeye alitaka kumaliza pambano kwa KO mimi nilicheza ngumi za akili raundi ya kwanza hadi ya tatu muda wote anakuja harudi nyuma,” anasema.

Anasema ilibidi atumie nguvu ya ziada kuhakikisha anakwepa ngumi za bondia huyo kwanza ndipo atafute nafasi ya kushambulia na akashinda kwa pointi.

Astaafu ngumi

Koba anasema aliamua kustaafu ili kuendelea kulinda heshima yake baada ya mwili kumgomea.

“Ndivyo inapaswa kuwa hata kwa mabondia wa sasa, ili heshima yako isishuke, unapaswa kustaafu wakati bado una uwezo kama nilivyofanya mimi mwaka 2000. Anasema kabla ya kustaafu, wakati huo kiwango kimeanza kupungua alipewa pambano la kushtukiza dhidi ya Mashaka Malulu.

“Ilikuwa mwaka 1997, nilishaanza kuchoka, nikaambiwa na kocha unajua kuna mechi keshokutwa tunacheza na Ngome (timu ya JWTZ) ubingwa wa mkoa na mpinzani wako ameletwa.

“Taarifa zile zilinistua lakini si unajua jeshini tena nikakubali nikijua sina mazoezi siku iliyofuata tukaenda kupima kwa ajili ya mechi ya siku pili.

“Ngome walikuwa wakimtambia Malulu walimtoa Mwanza ili aje kunipiga, alikuwa bonge la mtu, mimi na urefu wangu nilikuwa namuangalia kwa juu, nikawa najiuliza huyu jamaa anajua ngumi kiasi gani sababu simfahamu wala sijui uwezo wake.

Anasema wakati huo timu ya Ngome ilikuwa inanolewa na Nassor ambaye amecheza naye na anajua uwezo wake.

“Wakati huo ilikuwa kupigwa ni fedheha kila mtu alijua Koba anapigwa, nikawa najisemea mwenyewe hapa nikicheza ovyo nadhalilika kweli.

Anasema Malulu alimshambulia raundi yote ya kwanza bila majibu, kumbe yeye Koba alikuwa akimsoma raundi ya pili alimuotea ngumi moja ya kulia iliyotua kichwani jirani na paji la uso.

“Ile ngumi ilimpeleka chini hakuamka, alihesabiwa bila majibu refarii akamaliza pambano nikawa nimeshinda kwa Knock Out (KO) lakini mwenyewe sikuamini kama nimeshinda.

Anasema miezi mitatu baadaye walirudiana na Malulu ambaye alicheza kwa kiwango bora japo yeye Koba alishinda kwa pointi za majaji 4-1 na hilo ndilo likawa pambano lake la mwisho.

“Niliamua nistaafu maana kama ningelazimisha kuendelea kuna siku ningedhalilika na kushusha heshima yangu ulingoni sikutaka nifike huko

“Nikatundika glovu nikiwa kwenye kiwango nikaenda kusomea ukocha na kuwa kocha wa timu ya Polisi hadi nilipostaafu,” anasema.

Koba anayefahamika katika vijiwe vingi vya jijini, anasema licha ya kustaafu Polisi anaendelea kufundisha masumbwi na hivi sasa ni kocha wa mabondia wa gym ya Kwame ya Mburahati, Dar es Salaam.

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...