
London, England. Pep Guardiola amekubali kupoteza ubingwa jana Jumapili baada ya kuwafungia ndani wachezaji wake karibu saa nzima kufuatia kipigo cha mabao 2-0 walichopata kutoka kwa Tottenham Spurs.
Mabao ya Steven Bergwijn na Heung-min Son yalitosha kuipa Spurs ushindi dhidi ya wachezaji 10 wa Manchester City baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu Oleksandr Zinchenko, kipigo hicho kinamwacha Guardiola akiwa nyuma kwa pointi 22 dhidi ya vinara Liverpool.
Kocha huyo wa Etihad kwa mara ya kwanza amekubali kushindwa katika mbio zake za kuwania taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu England.
Guardiola alipoulizwa kama bado ananafasi ya kutetea ubingwa wake alisema: 'Wapo mbali sana hatuwezi kuwazuia. Wapo mbele kwa pointi nyingi, na sisi tumepoteza pointi kama ilivyokuwa leo.
“Lengo letu ni kushinda katika mashindano mengi yaliyobaki pamoja na kufuzu kwa hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao.'
City ilitawala mchezo huo kabla ya Zinchenko kupata kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu ndipo mchezo ulipobadilika.
Baada ya mchezo huo, Guardiola alijifungia na wachezaji wake katika vyumba vya kubadilishia nguo kwa zaidi ya dakika 50, wakizungumzu kuhusu kipigo hicho.
'Hapana, sijakasirika. Ni kawaida huwa sipendi iwe hivi kama hatuchezi vizuri, kama hatuwezi kukimbia au kupambana,' alisema Guardiola.
“Tunapopoteza mchezo siwezi kuwa mbali na wachezaji wangu kwa sabau nawajua vizuri. Lakini unapopoteza mchezo unazungumza nao kuhusu jinsi gani tutakwenda kuikabili michezo ijayo. Kuna mechi nyingi za kucheza mwezi huu.'
Guardiola pia alizungumzia kuhusu kauli aliyotoa mwenyekiti wa zamani wa Premier League, Richard Scudamore, ambaye alisema utawala City unaweza kuleta madhara kwa ligi hiyo baada ya kuchukua ubingwa kwa tofauti ya pointi 19.
'Misimu miwili iliyopita walisema City kutwaa ubingwa ni mbaya kwa Ligi Kuu England na jambo hilo halitatokea tena,' alisema kocha huyo City.
'Walisema kuna mtu anatakiwa kuisimamisha City isipate pointi 100, na kushinda tena ubingwa. Ila sasa ni Liverpool mnatakiwa kujiuliza kuhusu ubora wa Ligi Kuu.'
No comments:
Post a Comment