Search This Blog

Wednesday, January 22, 2020

Serikali ya mkoa wa kusini kupatiwa vitendea kazi

Na Thabit Madai,Zanzibar.

Serikali ya Mkoa wa Kusini Unguja imedhamiria kuwapatia wafanyakazi wa Mkoa huo vifaa vya kufanyia kazi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na ufanisi zaidi.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud ameeleza hayo wakati alipokuwa akiwakabidhi vyombo vya usafiri wafanyakazi  na viongozi wa wilaya ya Kati huko Halmashauri ya Wilaya Dunga.

Alisema lengo la kutolewa vifaa hivyo kwa wafanyakazi, ni kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi wa Wilaya ya Kati bila ya kupata vikwazo vya aina yoyte.

Amewataka wafanyakazi waliokabidhiwa vyombo hivyo kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa kwenda kwa wananchi kuwasikiliza na kuwasaidia katika kutatua changamoto zinazowakabili katika harakati zao za maisha.

Mkuu wa Mkoa amewasisitiza wafanyakazi hao kuhakikisha wanavitunza vyombo hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu hasa ukizingatia vimenunuliwa kwa gharama kubwa.

Aidhaa Ayoub ametoa tahadhari  kwa wafanyakazi wanaokusanya kodi waepukane na ubadhirifu na atakaebainika kufanya vitendo vinavyoenda kinyume na kazi hiyo atachukuliwa hatua za sheria bila kumuonea aibu.

“Natoa onyo kwa yeyote atakaeshiriki katika uvujishaji mapato atashughulikiwa wala hatoonewa haya , kwani katika jambo hilo sina mzaha wala sitomuoneya mtu muhali”, alisema Mkuu wa Mkoa wa Kusini.

Aliwataka wafanyakazi wa vituo vya afya vilivyomo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kati kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa  wanapofika vituoni kutaka huduma kwani lugha mbaya inaongeza machungu kwa mgonjwa.

“Nawaasa madaktari wenye tabia ya kuwatolea wagonjwa lugha zisizofaa wanapofika kwenye vituo wajirekebishe mara moja  wapeni moyo wagonjwa ili wapate faraja na muwape matibabu mazuri”, alisisitiza Ayoub.

Mkuu wa Wilaya ya Kati Hamida Mussa Khamis amesema lengo la kutolewa vyombo vya usafria kwa Wafanyakazi ni kuwawekea mazingira mazuri ya kutekeleza majukumu waliopewa ya kuwahudumia wananchi kwa wakati na ufanisi.

 Amewataka wafanyakazi hao kuthamini juhudi zinazochukuliwa na Serikali kwa  watendaji wa kada mbali mbali ili kuona wanaongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kati Said Mtaji Askari alisema kupatiwa vyombo vya usafiri wafanyakazi ni kutekeleza azma ya Serikali ya kuimarisha sekta ya Afya, Kilimo  na Elimu baada ya kufanyika ugatuzi ambapo hivi sasa baadhi ya shughuli zimehamishiwa katika Halmashauri za Wilaya .

Zaidi ya shilingi Millioni 100 zimetumika kununulia vyombo vya usafiri ikiwemo pikipiki tatu, vespa tano, pasola nane na gari moja la kubebea wagonjwa.

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...